Nabi akiri Kagera ilikuwa ngumu

KOCHA wa Yanga, Nasreddine Nabi

KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema kuwa kutokana na uchovu na aina ya uwanja, alijua kuwa mchezo dhidi ya Kagera Sugar utakuwa mgumu, lakini muhimu ni pointi tatu zilizowasaidia kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Vinara hao wa Ligi Kuu Bara wamekuwa na muendelezo mzuri wa kupata matokeo ikiwa ndio timu pekee ambayo haijapoteza mchezo hadi sasa ikiwa imeshuka uwanjani mara tisa ikishinda mara saba na kutoka sare mbili.

Akizungumza baada ya mchezo, Nabi alisema kutokana na kuwa na changamoto ya uchovu, ililazimika kufanya mabadiliko kwenye timu ndio maana hata uchaguzi wa kikosi ulizingatia zaidi wachezaji ambao wanaweza kucheza kwenye aina ile ya uwanja.

Advertisement

“Tunawaomba msamaha mashabiki wetu kwa kushindwa kuonesha mchezo mzuri, lakini tulikuwa tunahitaji pointi tatu vingine tutaenda kuvipanga mbele lazima tuwapongeze wapinzani wetu tuliocheza nao, wamecheza mchezo mzuri ilikuwa mechi nzuri jambo zuri tumetimiza malengo yetu,” alisema Nabi.

Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime alisema kuwa timu kubwa Simba na Yanga wana wachezaji  wanaotembea na matokeo, lakini waliuchukua mchezo na kutawala dhidi ya timu kama Yanga sio mchezo.

“Mpango wetu ulifanikiwa, lakini hatukuwa na bahati, tulitengeneza nafasi nyingi za kufunga tukashindwa kuzitumia, tumeangushwa na vitu vichache ambavyo tutaenda kuvifanyia kazi kwenye uwanja wa mazoezi naamini tutaimarika.”

“Tuliwasoma Yanga wanavyocheza basi tukakamata maeneo yao muhimu kama unavyoona tuliushika mchezo, nawapongeza Yanga kwa kupata pointi tatu na bao moja sisi mchezo ulikuwa wetu lakini hatukuwa na bahati,” alisema Maxime.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *