Nabi alia na ratiba Bara
BAADA ya kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Ihefu FC kwenye Uwanja wa Highland Estate, Mbarali mkoani Mbeya, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, amekiri kuwa ugumu wa ratiba ya Ligi Kuu Bara umechangia kupoteza mchezo huo na kuvunja rekodi yao ya kutopoteza.
Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya tisa lililofungwa na Yanick Bangala kwa kichwa akimalizia mpira wa krosi uliopigwa na Joyce Lomalisa na kuwapa uongozi vinara hao wa Ligi Kuu Bara.
Ihefu walisawazisha bao hilo dakika ya 39 lililofungwa na Never Tigere kwa mpira wa adhabu, kabla ya Lenny Kisu kuihakikishia ushindi timu yake dakika ya 69 akimalizia kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Tigere.
Akizungumza baada ya mchezo, Nabi alisema kuwa anawapongeza Ihefu kwa ushindi walistahili kwani walikuwa bora uwanjani na nidhamu yao ya mchezo ilikuwa nzuri.
“Hatukucheza vizuri, nidhamu yetu ya mchezo haikuwa nzuri, miili ya wachezaji ina uchovu mkubwa kuna wakati walikuwa hata wazito kukimbia. “Ratiba imekuwa ngumu sana kiasi cha kuchosha wachezaji, tumecheza takribani mechi nane ndani ya mwezi mmoja na tunasafiri sana muda mwingi ni mazoezi si ya kujenga miili na mifumo kutokana na muda,” alisema Nabi.
Alisema wakati mwingine vyema kupoteza mechi baada ya kutofungwa kwa muda mrefu ili kuirudisha akili katika mfumo wa upambanaji kutofungwa muda mrefu pia huchangia kuleta presha.
Kocha Mkuu wa Ihefu, Juma Mwambusi, alisema anamshukuru Mungu kwa kupata matokeo hayo na aliwaambia wachezaji wake waiheshimu Yanga, ni mabingwa wa kihistoria na wanaongoza ligi timu kubwa ambayo haijafungwa ila twendeni uwanjani tukacheze.
“Kila jambo lina wakati, nimeikuta timu katikati tunapoteza michezo kikubwa nilichofanya nilirekebisha baadhi ya mambo walikuwa wanapoteza mechi kwa kutotumia nafasi, nilikaa na wachezaji muda mrefu nikawaambia tunaweza kufanya kitu,” alisema Mwambusi.
Alisema aliwaambia vijana wake wacheze mpira wasibutue maana Yanga wana timu nzuri, wana wachezaji wenye uwezo kipindi cha pili walishambulia sana lakini alifanya mabadiliko ya kiufundi kwa kuingiza walinzi kwa ajili ya kulinda ushindi na kufanikiwa kuondoka na pointi tatu.