Nabi ataja siri ya ushindi
KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema siri ya timu yake kuendelea kupata ushindi katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara ni ubora wa kikosi chake na wachezaji kutambua wajibu wao wawapo uwanjani.
Yanga juzi ilikuwa ugenini Uwanja wa Liti mjini Singida dhidi ya Dodoma Jiji na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, matokeo ambayo yamewarudisha kileleni mwa msimamo wa ligi kwa kufikisha pointi 29 na michezo 11.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Nabi alisema waliingia kwenye mchezo huo wakijua wanakwenda kukutana na timu inayocheza kwa kutumia nguvu nyingi, lakini ubora na uzoefu wa wachezaji wake ndio vimechangia kuchukua pointi zote tatu.
“Niwapongeze wachezaji wangu japokuwa tumecheza kwenye mazingira magumu, lakini wamepambana na kupata ushindi pointi tatu ndiyo ilikuwa kitu muhimu ingawa haikuwa rahisi kutokana na uwanja kutokuwa rafiki sana,” alisema Nabi.
Kocha huyo pia ameendelea kulalamikia ratiba kuwa siyo rafiki na inawaweka katika wakati mgumu wachezaji wake kutokana na kukosa muda wa kutosha wa kupumzika kwa kucheza mechi mfululizo pasipo kupumzika.
Alisema hata kuumia kwa wachezaji wake wawili, nahodha Bakari Mwamnyeto na Feisal Salum kumetokana na kukosa muda wa kutosha wa kupumzika, jambo ambalo linaweza kuwaathiri na kushindwa kufanya vizuri mechi zijazo kwa kuwakosa baadhi ya wachezaji wao muhimu.
Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji, Melis Medo alisema kilichosababisha wakapoteza mchezo huo ni wachezaji wake kuingiwa na hofu na kushindwa kufuata maelekezo ambayo amewapa kabla ya mchezo huo.
Medo alisema walianza vizuri lakini baada ya wapinzani wao Yanga kuwazoea mchezo uliwabadilikia na kutoa nafasi kwa wageni wao kuwashambulia na kupata bao kabla ya mapumziko.
“Wachezaji wangu wameihofia Yanga, walishindwa kutekeleza maagizo niliyowapa ndio maana tumepoteza mchezo lakini nawapongeza Yanga kwa ushindi na sisi tunajipanga ili kufanya vizuri mechi zinazokuja,” alisema Medo.
Kipigo hicho kimezidi kuiweka katika nafasi mbaya Dodoma Jiji ambayo ipo nafasi ya 15 kwenye msimamo ikiwa na pointi tisa katika michezo 12 iliyocheza mpaka sasa.