Nabi awapa saluti wachezaji

Nabi akili nyingi mechi na Watunisia

KOCHA wa Yanga SC Nasreddine Nabi amesema anaridhika na kikosi chake kwa namna kinavyopambana kupata ushindi. Yanga juzi ilicheza mchezo wake wa pili wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union ya Tanga na kushinda kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa.

Huo ni ushindi wa pili kwa Yanga, baada ya kushinda mabao 2-1 katika mechi ya kwanza dhidi ya Polisi Tanzania. Akizungumza baada ya mchezo huo juzi, Nabi alisema walicheza na timu nzuri na walikuwa wanajua mechi itakuwa na ushindani. Alisema ni mechi ya tatu katika siku saba sasa hivyo unakuta mwili umechoka, uwanja pia sio rafiki sana hivyo vitu vinafanya mechi kuwa si rahisi.

“Lakini kitu cha kwanza wachezaji kujitambua na kujua umuhimu wa pointi tatu na umuhimu wa kila mechi ya ligi, tunaweza sema ni kazi kubwa maana kipindi cha pili baada kama dakika 15 hadi 20 tuliona Coastal Union walikuwa chini sana lakini sisi tukabaki na hali ile ile na tukamaliza mechi vizuri,”alisema Nabi.

Advertisement

Nabi alitoa pole kwa ajali ya mashabiki wao iliyotokea wakiwa safarini kwenda Arusha kushuhudia mechi hiyo ambapo shabiki maarufu Da Hadija alifariki. “Tulisema mechi ya leo (juzi) pia tucheze kwa ajili ya mashabiki wetu waliopata matatizo na tuoneshe kama tunawajali kama wanavyojitoa na sisi tunazitambua juhudi zao kwa timu yao tunawaambia poleni nasi imetugusa,”alisema Nabi.

Kwa upande wa kocha wa Coastal, Juma Mgunda alikiri timu yake kuzidiwa na kwamba huo ndio mchezo wa mpira ulivyo. “Tumeruhusu goli mbili kwa uzembe wetu walinzi wetu walifanya makosa ya kimchezo na kupelekea wachezaji ambao wanauelewa mzuri na uzoefu wa kutosha wakatuadhibu,”alisema Mgunda.