Nabi, Sabilo kocha, mchezaji bora Oktoba
KOCHA MKuu wa mabingwa watetezi Ligi Kuu Bara Yanga, Nasreddine Nabi na kiungo mshambuliaji wa Mbeya City, Sixtus Sabilo wameng’ara katika tuzo za Ligi Kuu ya NBC za mwezi Oktoba.
Katika kinyang’anyiro hicho Nabi amewashinda Abdallah Mubiru wa Mbeya City na Thiery Hitimana wa KMC alioingia nao fainali.
Nabi ameshinda tuzo hiyo ya mwezi Oktoba baada ya kuiongoza Yanga kukusanya pointi 10 katika michezo minne ikishinda mitatu dhidi ya Ruvu Shooting 2-1, KMC 1-0, Geita Gold 1-0 na kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Simba.
Kwa upande wa Sabilo ameshinda tuzo hiyo baada ya kuwabwaga Saido Ntibazonkiza wa Geita Gold na Dickson Job wa Yanga, ambao aliingia nao fainali katika kinyang’anyiro hicho.
Sabilo amehusika katika mabao matano ya mwezi Oktoba akifunga mawili na kutoa pasi tatu za mabao hii ni mara ya kwanza kwa kiungo mshambuliaji huyo wa Mbeya City kutwaa tuzo hiyo msimu huu.
Pia kamati ya tuzo imemchagua meneja wa Uwanja wa Sokoine Modestus Mwaluka kuwa meneja bora wa mwezi Septemba kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.