Nafasi maofisa utamaduni kujazwa

WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Dk Pindi Chana amesema wizara yake inafanya mazungumzo na Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kuangalia mahitaji halisi ya kujaza nafasi kwa maofisa utamaduni na michezo kwenye halmashauri mbalimbali nchini.

Waziri Dk Chana alisema hayo Agosti 17, 2023 mjini Morogoro wakati akifungua mkutano “ Re- Treat” kwa ajili ya menejimeti na watendaji wakuu wa wizara na taasisi zake .

Alisema hatua hiyo itarahisisha kuona namna ya kuomba vibari vya kuajiri watumishi wapya wa kada hizo kwa lengo la kujaza nafasi za wazi zilizopo Ili kuwawezesha maofisa hao kuteleza majumu yao ya kusimamia michezo na utamaduni kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Advertisement

“Wizara imeshatoa maagizo kuona ni namna gani katika kipindi hiki cha mpito wakati vibari vinasubiriwa vya kuajiri rasmi maofisa michezo na maofisa utamaduni , lazima kuwe na watu wanaoshikilia hizo nafasi kwa wao kukaimu ili shughuli ziendelee.” alisema Dk Chana

Dk Chana alisema Tanzania ina halmashauri za wilaya 184 , na hizo ni taaluma muhimu zinazochangia kujenga maadili mema ya Mtanzania na kuleta maendeleo endelevu ya taifa

Hivyo alizitaka halmashauri za wilaya na mikoa ambayo haina wataalamu wa kada hizo ziweke watu ambao watakaimu ili kazi iendelee.

“ Nimeshaanza mazungumzo na waziri wenzangu wa Tamisemi , Angellah Kairuki kuangalia tunahitaji kujaza nafasi ngapi na tuangalie tunapataje vibari vya kuajiri watumishi Maofisa Michezo na Maofisa Utamaduni” alisema Dk Chana

Dk Chana alisema, katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan, Watanzania wameshuhudia Tanzania inag’ara katika nyanja mbalimbali zikiwemo za Utamaduni, Sanaa na Michezo.

“ Huu ni mwanzo chini ya Rais Samia , mambo mengi ya kimkakati yanakuja na hiki kikao cha wizara ni mkakati wa kujipanga ni namna gani tutawafikia watanzania “ alisema Dk Chana

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *