JUMLA ya wanafunzi 1,929 wanaosoma katika taasisi za elimu ya juu zilizopo Zanzibar walipangiwa kupewa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 5.8 katika mwaka 2021/2022.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omari Kipanga alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Wete, Omari Ali Omari (CCM).
Omari alitaka kujua ni wanafunzi wangapi kutoka Zanzibar wamepata Mikopo ya Elimu ya Juu kwa mwaka 2020/2021.
Kipanga alisema serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imekuwa ikitoa mikopo kwa wanafunzi wote Watanzania wenye uhitaji bila kuangalia mwombaji anatoka upande upi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hivyo, takwimu za mwaka 2020/2021 zinaonesha kuwa wanafunzi Watanzania wapatao 1,492 wanaosoma katika taasisi sita za elimu ya juu zilizopo Zanzibar walipangiwa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 5.3.