Naibu waziri apiga vita imani potofu

NAIBU Waziri wa Madini, Dk Stephen Kiruswa amezitaka jamii ya kifugaji ya kimasai kushirikiana na kupiga vita imani potofu zinazolenga watoto kutojihushisha na elimu kwa madai kuwa yanaenda kinyume na maadili ya jamii hiyo.

Kiruswa alisema kuwa imani hizo zinapelekea vijana wengi wa jamii ya kifugaji ya kimasai kushindwa kumudu soko la ajira.

Kiruswa ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Longido mkoani Arusha alisema hayo katika sherehe za  kimila kwa jamii ya kifugaji ya kimaasai katika hatua ya kwanza kati ya hatua nne katika ukuaji wa vijana wa kabila hilo zenye lengo la kuwaimarisha vijana kimaadili.

Alisema na kusisitiza jamii hiyo kujitenga na imani hiyo potofu zilizoathiri mustakabali wa elimu kwa vijana wa jamii kifugaji na kujikuta iko nyuma kielimu.

‘’Wakati umefika kwa jamii ya kifugaji kupiga vita mila potofu za kupinga elimu kwani zimepitwa na wakati na sasa kila mmoja awe mstari wa mbele kuhakikisha vijana wadogo wakike na kiume kwenda shule na wazazi tuwaunge mkono’’alisema Kiruswa

Mkuu wa Wilaya ya Longido, Marco Ng’umbi alisema kuwa mikakati ya serikali katika wilaya hiyo ni kuboresha miundombunu ya sekta ya elimu kwa kuongeza ujenzi wa vyumba vya madarasa hivyo vijana wengi wanapaswa kwenda shule kwa maslahi ya nchi.

Ng’umbi alisema kuwa serikali imeshapeleka katika wilaya hiyo zaidi ya Sh bilioni 1.5 kwa ajili ya elimu hivyo ni lazima jamii hiyo ya kifugaji inapaswa kumuunga mkono Rais samia katika jitihada za elimu.

Kwa upande wao viongozi wa kimila kutoka kabila hilo wanakiri misingi duni iliyofanywa tangu awali katika elimu na hatua walizoanza kuchukua ili kubadilisha mtazamo huo katika jamii yao ili vijana waweze kunufaika na elimu hiyo.

Laigwanani Thomas Ngolupa alisema kuwa imani hiyo potofu waliyoikuta kwa wazee wa mila waliopita ndio ilifanya vijana wengi kugoma kwenda shule ila sasa wao kama viongozi wa mila hawanabudi kuhamashisha kuachana na milla hizo zenye kuwarudisha nyuma kielimu.

Alisema na kusisitiza kuwa kila kiongozi wa milla katika Wilaya ya Longido kuhakikisha wanapita kila kitongoji,kijiji na kata kuhakikisha wanatoa elimu ya jamii hiyo kuacha mila hizo potofu zilizowaacha nyuma kielimu.

Naye kiongozi mwingine wa mila ,Laigwanani Lucas Sanyai alisema kuwa wakati wa umuhimu wa elimu kwa jamii ya kifugaji ya kimasai umefika hivyo kila kijana anapaswa kwenda shule kwa maslahi ya jamii hiyo.Katika kipindi cha miaka 14 vijana wa jamii hiyo watapita katika hatua tatu muhimu kabla ya hatua ya nne ya tohara na kisha kuingia kwenye kundi la morani na kupokea jukumu la ulinzi na kushiriki katika maamuzi kwa jamii.

Habari Zifananazo

Back to top button