NAIBU Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamisi Mwinjuma amevipongeza vilabu vya Simba na Yanga kwa kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
Pongezi hizo amezitoa leo Juni 06, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu maswali kutoka kwa wabunge sambamba na kutoa maelezo katika kikao cha 41, mkutano wa 11 kujadili bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
“Mbali na kuipongeza Yanga kwa kufika fainali Shirikisho Afrika CAFCC lakini pia nichukue fursa hii kuipongeza Simba kwa kufika robo fainali mara kwa mara hadi kuwa kawaida sasa, ingawa naamini watavuka hilo na kufikia mafanikio ya kushangaza pia niwapongeze kwa kuwa bora kwa miaka mitano mfululizo hali iliyopelekea kupata nafasi ya kushiriki Super League (mashindano mapya ya vilabu vigogo Afrika).”
Hata hivyo, amechukua nafasi hiyo kuwapongeza Yanga kwa kwa kufika fainali ya Kombe la Shirikisho (CAFCC) na kushika nafasi ya pili baada ya matokeo ya jumla kuwa 2-2 hivyo kushika nafasi hiyo kutokana na kanuni namba 55 ya FIFA ya bao la ugenini.
Itakumbukwa, Jumamosi ya Juni 03, 2023 Yanga ilicheza mechi ya mkondo wa pili wa CAFCC nchini Algeria dhidi ya USMA na kushinda bao moja, ilhali mechi ya mkondo wa kwanza Mei 28, 2023 jijini Dar-es-salaam walifungwa kwa mabao 2-1.