Naibu Waziri awasha umeme Ilambo

NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amezindua na kuwasha umeme katika kijiji cha Ilambo wilayani Kilolo mkoani Iringa huku akiliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kufikisha huduma hiyo katika shule ya sekondari Ibumu ili kuwawezesha wanafunzi wake kusoma nyakati za usiku.

Amelipa shirika hilo hadi kufikia mwezi Januari, 2024 huduma ya umeme iwe imefika katika shule hiyo hatua aliyosema itasaidia kuharakisha maendeleo ya kitaaluma.

“Umeme ni muhimu sana kwa shule zetu kwa sababu ni nishati inayohitajika kwa shughuli mbalimbali za kufundishia na kujifunzia. Pia, hutoa uwezekano wa matumizi ya vifaa vya kielektroniki kama kompyuta na kuongeza ufanisi wa mchakato wa elimu na maendeleo ya wanafunzi,” alisema.

Kufika kwa umeme huo kumeelezwa na wananchi wengi kwamba kutachochea shughuli za biashara na viwanda vidogo vidogo vinavyohitaji nishati hiyo ambacho katika historia ya uhuru wananchi wake hawakuwahi kufikiria kupata huduma hiyo.

“Ni furaha iliyoje kupata huduma hii. Hata kwa jambo la kuchaji simu za mkononi tulikuwa tunalazimika kuzipeleka vijiji jirani vyenye umeme ili tusikose huduma ya mawasiliano,” alisema mmoja wa wananchi wa kijiji hicho Richard Mtove.

Mtove aliipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuusimamia vyema mpango wa kupeleka umeme katika kila kijiji nchini akisema utaimarisha maisha ya kila siku vijijini, mawasiliano na utachochea shughuli za ujasiriamali na zingine nyingi za kijamii.

Wnanchi wengi wa kijiji hicho wameishukuru Serikali ya awamu ya sita na wamemuomba Dk Samia maisha marefu wakisema wanaona na kuthamini juhudi zake za kuliletea Taifa maendeleo katika nyanja mbalimbali.

“Ninashukuru umeme umefika nikiwa bado kijana.

Ni wajibu wangu sasa kwa kupitia akiba niliyonayo kutanua wigo wa shughuli zangu za kiuchumi. Nitafungua duka la kunyoa nywele, kuchomelea hata banda ya kuonesha mpira,” alisema Jeton Kivenuke ambaye kwasasa anajishughulisha na kilimo.

Akiwasha umeme katika moja ya nyumba zilizounganishwa na nishati hiyo kijijini hapo Kapinga amesema serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza mradi wa usambazaji umeme vijijini katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo vituo vya afya, taasisi za elimu, dini, masoko, visima vya Maji na mashamba.

“Niwatoe hofu wananchi, Rais Dk Samia Suluhu Hassan amekwishatoa maelekezo yanayotaka wananchi wote wafikiwe na huduma hii.

Sisi wasaidizi wake tupo kazini na ni kazi yetu kuhakikisha maelekezo hayo tunayatekeleza hatua kwa hatua.” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button