Naibu Waziri Byabato atoa maelekezo Miradi Mwanza
MWANZA; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Stephen Byabato, anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki amewataka watendaji na wasimamizi wa utekelezaji wa programu na miradi mbalimbali katika Jiji la Mwanza kupitia Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) kuhakikisha inatekelezwa kwa kasi na ufanisi, ili iwanufaishe wananchi wenye uhitaji.
Naibu Waziri Byabato amebainisha hayo wakati akiendelea na ziara ya kikazi ya ukaguzi wa ufanisi wa programu na miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Kanda ya Ziwa kupitia LVBC.
“Nitoe rai kwenu watendaji na wasimamizi wote wa miradi hii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inayotekelezwa katika Kanda ya Ziwa kupitia LVBC, kuhakikisha sote kwa umoja wetu tunafanya kazi usiku na mchana kutimiza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kuona wananchi wa Tanzania wananufaika moja kwa moja na fursa zinazotokana na Jumuiya kijamii na kiuchumi,” amesema Naibu Waziri Byabato.
Akiwa jijini Mwanza, Naibu Waziri Byabato ametembelea mradi wa ujenzi wa miundombinu ya majitaka na usafi wa mazingira chini ya programu ya pamoja ya usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji (LVB – IWRMP) katika eneo la Pasiansi.
Progamu hii inalenga kuchangia katika usimamizi endelevu wa rasilimali za maji ya Ziwa Victoria, ili kuongeza ubora na upatikanaji wake kwa matumizi mbalimbali, ikihusisha usambazaji wa majisafi kwa kaya zilizopo maeneo ya milimani na ujenzi wa miundombinu ya majitaka na vyoo vya kisasa.
Maeneo mengine yanayotarajia kunufaika na programu hiyo katika Jiji la Mwanza ni pamoja na Kitangiri, Mabatini, Kirumba na Nyamanoro.
Programu na miradi mingine aliyozitembelea jijini Mwanza ni pamoja na; ujenzi wa Makao Makuu ya Kituo cha Uratibu wa Utafutaji wa Uokozi katika Ziwa Victoria (MRCC), Ukarabati wa Meli ya Utafiti ya Jumuiya (RV Jumuiya) iliyopo Ziwa Victoria katika Bandari ya Mwanza Kusini unaofanywa na Kampuni ya kitanzania ya Mundao Engineering na eneo la Machinjio lililopo Nyakato ikiwa ni sehemu ya Programu ya Usimamizi wa Mazingira katika Ziwa Victoria.