Namna ya kufanya mbwa asile chakula cha adui

DAR ES SALAAM; MIONGONI mwa mambo muhimu katika ufugaji wa mbwa bora kwa ajili ya ulinzi, ni pamoja na kumpa mbwa nafasi ya kutembea na kuona mazingira mbalimbali akiwa chini ya uangalizi ili kumwondolea uzubaifu.

Katika mazungumzo na HabariLEO hivi karibuni, Dk Egyne Emmanuel ambaye ni mtaalamu wa mifugo anasema hali hiyo inamfanya mbwa achangamke.

Anasema mengine muhimu ni pamoja na kumfanyia mbwa usafi wa mara kwa mara ikiwa ni pamoja na kumwosha kwa dawa maalumu na kumpa tiba au dawa au chanjo dhidi ya maradhi mbalimbali ukiwamo ugonjwa wa kichaa cha mbwa.

Advertisement

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, mambo mengine muhimu ni kuhakikisha mbwa anafugwa katika banda lenye usafi na nafasi ya kutosha kutembeatembea ndani ya banda linalomwepushia kunyeshewa mvua na kupigwa jua.
Wataalamu wa ufugaji mbwa wanasema moja ya sifa za mabanda bora kwa ajili ya ufugaji wa mbwa, ni kumwezesha mbwa kuona mazingira ya nje.
Katika mazungumzo ya pamoja kuhusu namna ya kupata mbwa bora yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Kikosi cha Mbwa na Farasi Tanzania Kurasini, Dar es Salaam mwaka jana, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Khadija Maulid; Sajenti Dk Jabir Omar; Koplo Maulid Simba na Koplo Burhan Kimati waliliambia HabariLEO kuwa, yapo mambo kadhaa ya kuzingatia ili kupata mbwa bora yakiwamo mafunzo kwa mbwa, lishe bora na huduma bora za afya kwa mbwa.

Wakasisitiza kuwa, mbwa bora aliyefunzwa, kulishwa na kuhudumiwa sawia kiafya, hufanya kazi kwa tija, hufuata maagizo, hatoki kwenye lindo na hawezi kushambulia wanafamilia.

Wanasisitiza kuwa, mbwa wazuri wanaosisitizwa kufugwa katika familia ni hasa aina ya ‘Berigium-Malnoise’, ‘German Shepherd’ na ‘Alsation’ kwa kuwa wanapokea maelekezo haraka na kwa usahihi.

Kwa nyakati tofauti, Dk Emmanuel na wataalamu hao wa Kikosi cha Mbwa na Farasi Makao Makuu wanasisitiza mambo muhimu ambayo raia anaweza kufundishiwa mbwa wake ili awe mbwa bora kuwa ni pamoja na hasa ulaji sahihi na utii.

Khadija anasema familia inayofuga mbwa lazima imfanye mbwa wao kuwa sehemu ya familia.

Dk Jabir anaungana na Khadija akisema: “Ni muhimu wanafamilia wakiwamo watoto kupata muda wa kujenga uhusiano na mbwa wao kwa kumpa chakula kwa wakati sahihi na kucheza naye ili awazoee maana mbwa wengine usipomwonesha upendo hakupendi na hakutambui…”

Uzoefu katika maeneo mbalimbali nchini unaonesha kuwa, wafugaji waliojenga kasumba ya baadhi ya wanafamilia pekee kuzoeana na mbwa kwa michezo na huduma mbalimbali kama kumpa chakula, wamekuwa wakikumbana na changamoto ya mbwa wawafugao kuwashambulia baadhi ya wanafamilia.

“Kuna mahali pengine utakuta mama, mzee au baadhi ya watoto katika familia yao wanamwogopa mbwa wao maana akiwaona anawabwekea kwa ukali…”

“Hii ni kwa kuwa hajawazoea maana hawapati nafasi wala muda wa kucheza na kuzoeana naye na sababu nyingine ni kwamba, katika familia hizo anakuwa mtu mmoja pekee au wawili ambao ndio wanaompa chakula mbwa kila siku hivyo hao wengine anawaona kama wageni katika familia,” anasema Chacha Igotti, mkazi wa Pugu Kajiungeni, nje kidogo ya Dar es Salaam ambaye pia ni mfugaji wa mbwa kwa ajili ya ulinzi wa nyumbani.

Kuhusu chakula, Dk Jabiri na Dk Emmanuel ambaye ni mwandishi wa kitabu cha Bustani ya Mbwa ambacho kipo mbioni kuingia sokoni kwa nyakati tofauti wanasema, muda mzuri wa kumpa mbwa chakula ni saa tatu kabla ya kufunguliwa kufanya kazi ili muda huo autumie kupumzika.

Kuhusu namna ya kumlisha mbwa, Dk Jabir anasema: “Mfugaji ajenge utamaduni wa kulisha mbwa bandani na si mahali popote na walishwe washibe.”
“Mbwa akizoea kula akiwa bandani, kwenye chombo chake cha chakula na cha maji kwa muda maalumu, si rahisi kula chakula kwa kuokota hata kama atarushiwa na wenye nia mbaya.”

Dk Emmanuel anasema: “Mbwa akizoea chombo chake, hata ukimbadilishia chombo hawezi kula…”

Wadau mbalimbali wa ufugaji mbwa bora wanasema kwa kuwa mbwa ni mlinzi hivyo, lazima atengewe bajeti yake na kwamba si sahihi kumpa mabaki ya chakula kilicholiwa na watu mbalimbali yakiwamo mabaki kutoka hotelini au kwenye baa kwani ni rahisi kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali.

Sehemu ya Muswada wa Bustani ya Mbwa inazikosoa baadhi ya familia kwa kutojali umuhimu wa kuwa na bajeti iliyotengwa kwa ajili ya chakula cha mbwa wakidhani akiokota makombo yanayotupwa kutoka mezani, yatamtosha.

Kinasema: “Mfumo huu wa ulishaji mbwa si sahihi kwa sababu makombo hayapimwi kulingana na mahitaji ya mwili na kuwepo uwezekano wa kushinda na njaa au kula chakula kingi kupita kiasi kutokana na njaa ya muda mrefu, hivyo kupata athari.

Mwandishi Bustani ya Mbwa (Dk Emmanuel) anasema: “Makombo yanaweza kuambatana na takataka na hata kukusanywa na vitu vya kufisha hivyo kuleta madhara kwa mbwa.”

Anaongeza: “Mbwa anayetegemea makombo mara nyingi atashinda njaa pindi mapishi yanapokuwa hayakufanyika kwa sababu mbalimbali zikiwamo za kwenda kwenye sherehe au hotelini.”

“Sababu nyingine ni kwamba, mlo wa mbwa una tofauti kidogo ukilinganisha na mlo wa mwanadamu. Mbwa anatoka katika kundi la jamii ya walao nyama, yaani Carnivorous wakati binadamu anatoka katika jamii ya walao nyama na nafaka yaani Omnivorous.”

Kwa msingi huo anasema, ikitokea mlo unajumuisha sehemu kubwa ya mazao ya mimea kama vile mahindi na maharage (makande), wali na maharage, ugali na mbogamboga, chapati na maharage n.k, mbwa atapata tabu ya kula na pengine hatakula kabisa.

Ni vema mbwa akatunzwa vema na kutumiwa vyema kwa manufaa ya jamii.

Mfugaji mmoja wa mbwa anayekataa kutajwa gazetini anasema kumlisha mbwa makombo yakiwamo ya hotelini au kwenye sherehe, kuna mweka mbwa katika hatari ya kuambukizwa magonjwa mbalimbali na hatari ya kukumbana na vitu vyenye ncha kali katika chakula au vifuniko vya soda jambo ambalo ni hatari kwa mbwa.