Nape aitaka Posta kuongeza ubunifu kwenye biashara

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameagiza viongozi na watumishi wa Shirika la Posta Tanzania waongeze jitihada katika kubuni biashara za kiposta zitakazoendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia. Nape pia amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Jim Yonazi akomeshe urasimu unaodaiwa kuwapo katika taasisi kwenye wizara hiyo. Alitoa maagizo hayo Dar es Salaam jana wakati akizindua miradi ya Shirika la Posta ukiwamo wa Posta Kiganjani na Stempu ya Ushirikiano wa Pamoja kati ya Tanzania na Oman. Alizindua miradi hiyo katika Maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani. Nape alisema miradi hiyo ni muhimu kutokana na kusajiliwa katika mfumo wa malipo wa serikali hivyo itakuwa ni chanzo cha mapato ya serikali na alilishukuru shirika hilo kwa kufanikisha usajili wa anuani za makazi. Alisema miradi hiyo itakuwa na manufaa kwa kuwa kuna soko kubwa Tanzania kwa sasa la watumiaji wa simu wanaofikia milioni 58 ambapo kati ya hao milioni 37 wanafanya manunuzi kwa kutumia simu za mkononi hivyo Posta Kiganjani itakuwa na wateja wengi na wa uhakika. Nape alisema serikali haitavumilia wanaokwamisha mipango ya serikali kwani kufanya hivyo ni kukwamisha juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan. Dk Yonazi alisema mageuzi yanayoendelea katika utoaji wa huduma za posta yameliwezesha shirika hilo kuwa mfano wa kuigwa katika Kanda ya Afrika Mashariki na Kati.

Alisema mageuzi hayo yanalenga kulifanya shirika hilo kuwa chanzo cha kuaminika cha mapato nchini pamoja na kuwa chombo cha kila mwananchi ndani ya nchi ambacho kitasimama na kuwezesha uchumi wa kidijiti.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Moshi Suleiman Kakoso alisema Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imekuwa ya kisasa kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na waziri wake Nape Nnauye na kwamba wizara itamkumbuka kutokana na kazi nzuri ya kuigwa aliyoifanya ya Anuani za Makazi na Postikodi.

Aliitaka wizara hiyo kusimamia vizuri Shirika la Posta ili kuliwezesha kujitegemea na kusaidia pia kuondoa urasimu unaosumbua taasisi za serikali ndani ya wizara ili kuimarisha utendaji na kuongeza ubunifu.

Posta Masta Mkuu, Macrice Mbodo alisema Siku ya Posta duniani ilianzishwa miaka 148 iliyopita na kwa mara ya kwanza mwaka huu Tanzania inaadhimisha siku hiyo kwa kushirikiana na Oman chini ya kauli mbiu ‘Posta ni ya Kila Mtu’.

Alisema shughuli za posta zinaonesha ni za kila mtu kwa kuwa zinagusa nyanja zote za maisha ya mwanadamu ukiwemo usalama, viwanda na biashara, elimu, afya, uchumi, usafirishaji pamoja na utalii na kwamba kwa sasa posta ni zaidi ya barua. Naibu Balozi wa Oman nchini, Rashid Almanji alisema Serikali ya Oman itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya kiposta na nyanja zote za kiuchumi.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba alisema kuna mageuzi yamefanyika katika sekta ya posta kwa sasa ikilinganishwa na zamani.

Aliwasihi wafanyakazi wa shirika hilo wafanye kazi kwa bidi ili uwekezaji wa serikali katika shirika kuliwezesha liwe la kisasa uwe na tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Habari Zifananazo

Back to top button