WIZARA ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema tangu Oktoba mwaka jana gharama za mawasiliano nchini hazijaongezeka na pia kiwango cha bando hakijapunguzwa.
Waziri wa wizara hiyo, Nape Nnauye alisema hayo bungeni Dodoma wakati anachangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha 2023/24 na kujibu hoja za wabunge.
Nape aliwaeleza wabunge kuwa wanaosema gharama zimepanda wanapotosha kwa kuwa kwa miezi tisa hakuna gharama za mawasiliano zilizoongezeka.
“Kuna hatua zilichukuliwa na ndio maana hali ikatulia, Serikali ya Awamu ya Sita ilichukua hatua ya kutuliza gharama zisiendelee kupanda,” alisema.
Nape alisema hatua ya pili ilikuwa ni kuzishusha gharama hizo na akasema gharama za uwekezaji kwenye miundombinu zinachangia ukubwa wa gharama za mawasiliano.
“Watu wa mawasiliano tulikuwa tunalipa dola 1,000 kwa kilomita kwa mwaka tukipitisha miundombinu ya mawasiliano kwenye road reserve (hifadhi ya barabara), lakini mapendekezo yaliyoletwa kwenye bajeti hii ni kuitoa dola 1,000 kwa mwaka kepeleka dola 100 kwa mwaka,” alisema.
Nape alisema pendekezo hilo litapunguza gharama za uwekezaji na akasema pia gharama za mawasiliano zinasababishwa na gharama za uendeshaji.
Alitoa mfano kwamba mnara unaotumia mafuta ya dizeli unaendeshwa kwa Sh 1,800,000 kwa mwezi lakini ukitumia umeme unaendeshwa kwa Sh 400,000.
“Bajeti hii imeelekeza upelekaji wa umeme kwenye vitongoji na Rais alielekeza kwamba umeme huu ukipelekwa uende ukaweke kipaumbele kwenye maeneo ya mawasiliano…na hizo ndio hatua ambazo zitashusha gharama za mawasiliano katika nchi yetu,” alisema Nape.
Nape alisema kodi kwenye huduma za mawasiliano bado zipo juu kwa kuwa katika kila Sh 100 inayolipwa Sh 41 inakwenda kwenye kodi hivyo wizara anayoiongoza itaendelea kuzungumza na Wizara ya Fedha na Mipango waendelee kufanya mapitio kwa kuzingatia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Pia aliwaeleza wabunge kuwa anapongeza pendekezo la serikali katika bajeti yake la kuwa na uchumi usiotumia fedha taslimu.
Nape pia alipongeza kutengwa fedha za kuwekeza katika sekta ya mawasiliano zikiwamo za mkongo wa taifa kuiwezesha nchi kuwa na mawasiliano ya uhakika.
Alimpongeza Rais Samia kwa uamuzi wa kujenga nchi yenye kupenda haki kwa kuunda timu ya kukusanya maoni yenye lengo la kuboresha haki jinai nchini.