DAR ES SALAAM: Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amemuelekeza Katibu Mkuu katika Wizara hiyo, Mohammed Khamis Abdulla kuunda timu itakayoshirikiana na watendaji katika Kampuni ya Magazeti ya Serikali Tanzania (TSN) kuharakisha ujenzi wa kiwanda cha uchapaji kinachojengwa jijini Dar es Salaam.
Nape ametoa maelekezo hayo leo Machi 7 wakati wa kikao chake na Menejimenti ya TSN na baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo akitaka timu itakayoundwa iwe na jukumu la kufuatilia mwenendo wa ujenzi na kutoa ripoti kwa Waziri kila wiki.
“Ujenzi huu tunataka ukamilika kabla ya mwezi wa sita. Kama Wizara tutazungumza na wenzetu wa Wizara ya Fedha kuwezesha mtiririko wa fedha,” amesema Waziri Nape. Ujenzi wa kiwanda hicho cha kisasa unakadiriwa kugharimu zaidi ya Sh bilioni 30. Ujenzi wa jengo unatekelezwa na Mkadarasi Group Six.
Waziri Nape amesema amepanga kukutana na Mkandarasi (Group Six) leo ili kukubaliana namna bora ya kukamilisha ujenzi huu. Ujenzi huo ulioanza Juni Mwaka jana, ulipangwa kukamilika mwezi Disemba 2023. Kwa sasa, ujenzi huo umefikia asilimia 30 na unatarajiwa kukamilika Juni 2024.