Nape ataka habari za kufichua maovu

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewataka waandishi wa habari nchini kutumia vyema taaluma yao na kujikita katika habari za uchunguzi ili kufichua maovu hali itakayosaidia serikali kufanya maamuzi sahihi.

Pia, ameelezea kusikitishwa kwake na namna baadhi ya vyombo ya habari hususani vya mitandao vinavyoripoti taarifa za uzushi ili tu kupata watazamaji wengi au kwa sababu za mrengo wa kisiasa na kusisitiza hakuna uhuru usio na mipaka.

Nape aliyasema hayo jana wakati akihojiwa na Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dk Ayoub Rioba kwenye kipindi cha Mizani kinachorushwa na televisheni hiyo.

Alisema vyombo vingi vya habari haviripoti habari za uchunguzi hali ambayo imewafanya watu wengi kuanza kupoteza hamu ya kusoma au kusikiliza habari kwa sababu taarifa nyingi zinazoandikwa ni zile tayari zimeshaonekana kwenye mitandao ya kijamii.

Nape alisema kuna haja vyombo vya habari sasa kuwekeza katika uandishi wa uchunguzi kwa kuwawezesha waandishi wa habari kusafiri mbali kwenda kuchokonoa mambo na kuja na habari zenye tija. “Rais Samia amepeleka mabilioni ya hela, lakini mpaka ukisikia ziara za viongozi ndio unasikia kuna mchwa, sasa mtu ukijiuliza hawa mchwa mpaka wanachukua hela wanakula, waandishi wa habari wako wapi?

Kuna jambo haliko sawa,” alisema. Pia, alisema jambo lingine linalosababisha kukosekana kwa habari za uchunguzi ni ukosefu wa ari kwa mwandishi wa habari.

“Zamani mwandishi wa habari za uchunguzi alikuwa anajivunia na hata ukimuona ana hadhi fulani. Lakini sasa hivi si kuandika hata anayetangaza, unaweza kuulizwa swali hadi wakati mwingine wewe unayeulizwa inabidi umsaidie kuuliza ili apate stori,” alisema.

Alisema ni dhahiri kuwa kwa sasa watu wengi wanalalamika wakihoji ziko wapi habari za kiuchunguzi.

“Wanahoji liko wapi gazeti ambalo unaliweka Jumapili litoke nisome, ziko wapi stori za series (mtiririko) zimefanyiwa utafiti kesho unatafuta ili uendelee ilipoishia?”

Alitolea mfano uchaguzi uliomalizika nchini Kenya kuwa ni mwandishi gani ambaye ataleta habari zaidi ya uchaguzi.

“Pia kule tunaotokea Kusini korosho zinaingiza hadi shilingi trilioni 1.3 lakini fedha hizi haziendani na wananchi wanaolima hizo korosho. Kuna mtu anapata fedha hadi karibu bilioni moja, lakini utashangaa inapofika msimu wa kuandaa shamba hana hela ya kusafisha wala kuandalia. Sasa hebu tuchimbue tujue hawa hela wanapeleka wapi?” Alihoji.

Alisema anaamini kuwa habari za uchunguzi zikitafutwa nchini zipo na kwamba endapo waandishi wa habari wakijikita zaidi kwenye habari za uchunguzi wataisaidia serikali kufanya maamuzi sahihi.

Kuhusu uhuru wa vyombo vya habari na uandishi wa habari za uzushi, Waziri huyo alisema hatua zimechukuliwa za kuboresha mazingira ya uhuru wa habari nchini.

“Uhuru wowote una mipaka, ukimuingilia mwenzako ni tatizo. Sheria zimewekwa ili kudhibiti hilo, mtu atafute habari aichakate bila kumbughudhi mwenzake. Uhuru wako unapoishia ndipo uhuru wa mwingine unapoanzia,” alieleza.

Alisema katika zama za kiteknolojia za sasa, uhuru ambao ulikuwa unatosha jana unaweza usitoshe leo. Lakini pia uhuru ambao jana ulikuwa mkubwa sana leo ukiuachia sana unaweza ukamuingiza mtu kwenye matatizo.

Kuhusu upotoshaji alikiri kuwa upo, na kwamba hata yeye mwenyewe tangu amekuwa Waziri wa Habari amechukua hatua kadhaa ikiwemo kuwaita baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari ili kujua sababu za upotoshaji wao.

“Hivi karibuni Mwakyembe (aliyekuwa Waziri wa Habari Dk Harrison Mwakyembe) aliwasiliana na mimi na kunieleza kuwa kuna chombo kiliandika anaumwa, kafa na hadi mazishi yake wakati yuko hai. Sasa tunajiuliza msingi wake nini unakaa mpaka unatunga uongo,” alisema.

Aidha, alisema hata katika msiba wa Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli, kulikuwa na televisheni kama hizo zilizoandika habari nyingi za uzushi kuhusu kiongozi huyo.

“Ni kweli tumechukua hatua za kupanua wigo, televisheni za mtandaoni zilizofungiwa karibia zote tumeziachia tukasema hawa pengine tayari watakuwa wamejifunza. Na kila tunapowaita tuliwaelimisha. Bahati mbaya baada ya kufunguliwa zikaongezeka, nina orodha ya hizo televisheni zenye taarifa feki,” alisema.

Alisema katika kufuatilia na kuwabana baadhi yao, walieleza kuwa wanafanya hivyo ili kupata watazamaji wengi kwa kuwa ukiwa na watazamaji wengi unalipwa, wengine sababu za mrengo wa kisiasa na wengine ni sababu za ushamba tu.

“Leo nimemuuliza mmoja kwamba hivi utatangaza hizi habari moja mpaka tatu bila serikali kukuuliza? Kwanini usitafute namna nzuri ya kufanya.

“Wapo ambao wanatangaza uongo tu wa kawaida wa huko mtaani unamuambia hatutaki kufungia huwezi kubadilisha maudhui mbona wapo wengi wana watazamaji na wanahabari za kawaida tu,” alisema.

Nape alisema pamoja na nia njema ya serikali kuongeza uhuru, kurahisisha ufunguaji wa hivyo vituo, kupanua wigo wa kutoa leseni lakini imekuja pamoja na madhara. “Mzee Mwinyi aliwahi kusema unaweza kufungua dirisha upate hewa wakaingia pamoja na mbu sasa sisi tunajaribu kuweka nyavu tupate hewa lakini mbu na nzi wabaki nje,” alisema.

 

Habari Zifananazo

Back to top button