Nape: Heshima na utu wa watu ni jambo la msingi

DAR ES SALAAM: Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema wakati dunia inajenga uchumi wa kidijitali uliozifanya taarifa kuwa bidhaa muhimu, kuzingatia faragha, heshima na utu wa watu ni jambo la msingi.

Nape ameyasema hayo leo Aprili 03, 2024 katika uzinduzi wa  Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Amesema,  umuhimu wa Tume hiyo ni  kulinda maslahi ya wawekezaji ndani na nje ya nchi ili  wawekeze kwa tija.

Advertisement

“Tume inatarajiwa kuimarisha misingi ya demokrasia, utawala bora na utawala wa sheria, mazingira haya yatavutia uwekezaji wa ndani na nje kwani wawekezaji watakuwa na uhakika na uwekezaji wao,” amesema

Aidha, amesema  utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa taarifa binafsi nchini, utasaidia wawekezaji wa ndani kupata fursa sawa katika kuwekeza katika nchi zingine kwani watakuwa wanaaminika kutokana na nchi yetu kutekeleza makubaliano ya jamii ya kimataifa ya kuwa na sheria hiyo.