WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye anatarajia kuwa mgeni rasmi kwenye tamasha la Pasaka litakalofanyika April 9,2023.
Tamasha hilo litafanyika bure katika viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya maaandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama amesema Waziri Nape amekubali kuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo ambalo litafanyika baada ya kusimama kwa miaka sita.
Amesema, kamati yake inaendelea na maandalizi ya kuelekea tamasha hilo ambalo litashirikisha waimbaji mbalimbali wa ndani na nje nchini.
“Maandalizi kuelekea Tamasha la Pasaka yanaendelea vema, hivyo wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mikoa ya jirani ya Pwani na Morogoro wakae ya wajiandae kupokea ujumbe wa neno la Mungu kupitia viongozi wa dini na waimbaji wa muziki wa Injili,” amesema
Msama ametaja wasanii ambao watatumbuiza kwenye tamasha hilo kutoka nje ni Masi Masilia kutoka Congo Faustine Munishi kutoka Kenya, Tumaini Akilimali kutoka Kenya, Joshua Ngoma kutoka Rwanda na Nicole Ngabo kutoka Congo
Aidha, kwa upande wa wasanii wa injili wa hapa nchini watakaopamba tamasha hilo ni John Lissu, Upendo Nkone, Mashamsham Band na Kwaya ya Uinjilisti Kijitonyama.
Amesema, waimbaji wote wapo tayari na kwamba tamasha la mwaka huu sio la kukosa.
Advertisement
“Wakazi wa Dar na Mikoa ya jirani waje kwa wingi, tamasha hili halijafanyika muda mrefu takribani miaka sita, usalama ni wa hali ya juu, tutashirikiana na Jeshi la Polisi.” Amesema
Amesema mazoezi ya kutumia vyombo vya muziki yanaendelea kwa wasanii wa ndani ambao wamewatangaza kushiriki tamasha hilo ambalo siku hiyo wataimba ‘live’ na sio kutumia CD.