Nape: Rais alinisihi kuacha kubishana mitandaoni

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Rais Samia Suluhu Hassan alimsihi kuacha kujibizana na watu mitandaoni na badala yake asimamie falsafa ya R4.

Nape ameyasema hayo leo Machi 27, 2024 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, katika kilele cha kurasa 365 za Mama zikiangazia mafanikio ya Rais Samia tangu alipoingia madarakani Machi 19, 2021.

Nape amesema mara kadhaa Rais Samia huchafuliwa lakini amekuwa kimya huku asisitiza yasichukuliwe maamuzi yatayowadhuru raia wengine.

Advertisement

“Kuna wakati fulani, kuna jamaa fulani walimshambulia sana Rais na familia yake kwenye mitandano, huku ndani wakaanza kusema sasa waziri tunafanyaje? Mjadala ukawa mkubwa tuwachukulie hatua, tena kali!

Tukasema kwa hawa au kwa jukwaa lote lililotumika?

“Lakini wakati majadiliano yakiendelea, habari zilivuja na kumfikia Rais Samia ambaye aliamua kuniita na kuniambia nataka utatue jambo hili kwa busara,” amesema Nape na kuongeza

“Mama akaniita bana, akaniambia Nape…nimesikia mnajadiliana, lakini naomba nikukumbushe, nilitangaza 4R, mojawapo ni kuvumiliana, akasema hata kama mnataka kufanya lolote, hakikisheni hamuingilii uhuru wa watu kujieleza,” amesema

R4 za Rais Samia ni maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga taifa.