WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Serikali ya Awamu ya Sita ni sikivu ndio maana ilishusha tozo ya miamala ya simu kwa zaidi ya asilimia 50.
Nape amesema hayo alipozungumza katika kipindi cha Dira ya Dunia kilichorushwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Alisema malalamiko ya sasa kuhusu tozo yanatokana na kutoeleweka tofauti ya tozo zikiwemo zinazosimamiwa na wizara yake na tozo za miamala ya kibenki.
Nape alisema tozo za miamala ya kibenki zitazungumziwa na Wizara ya Fedha na Mipango ila anadhani kuna kutokueleweka zikiwemo hisia kwamba mtu anatozwa kodi mara mbili au mara tatu.
Alisema tozo za miamala ya simu zimepunguzwa kwa zaidi ya asilimia 50 ili kuruhusu wananchi waendelee kuitumia miamala hiyo kwa mambo mbalimbali.
“Huu ni ushahidi kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inasikiliza. Kulikuwa na kelele, tukarudi bungeni, tumepitia upya, tumepunguza kwa zaidi ya asilimia 50,” alisema Nape.
Hivi karibuni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema serikali inatambua kuwepo madai kuhusu tozo hizo lakini kuna upotoshaji hivyo serikali itatoa ufafanuzi ili Watanzania waelewe nini kimefanyika.
Kuhusu maslahi ya waandishi wa habari alisema mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 yatahusu pia maslahi ya kundi hilo zikiwemo bima kwa kuwa wanafanya kazi katika mazingira magumu.
“Lakini pia tuone namna ambayo tutawabana pia wamiliki wa vyombo vya habari watoe maslahi mazuri. Leo Tanzania ni katika nchi ambazo habari za kiuchunguzi zimeshuka sana lakini msingi wake ni mmoja tu ukitaka kufanya habari za kiuchunguzi lazima uwekeze. Watu waende,” alisema Nape.
Pia alisema moja ya malengo ya kutungwa kwa sheria ya mwaka 2016 ni kupunguza mikono ya serikali katika kuendesha vyombo vya habari.
“Sheria hii tukatamani ipunguze na namna ya kupunguza ilikuwa ni pamoja na kuunda Baraza Huru la Wanahabari ili yale ya kitaaluma wayamalize huko,” alisema Nape.
Aliongeza: “Tuliamini ukishafanya hivyo, maana yake umeondoa madaraka kwa Mkurugenzi wa Habari Maelezo. Lengo Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo ambaye ndiye mwakilishi wa serikali katika kusimamia vyombo vya habari, tunataka madaraka yake yapungue kadri inavyowezekana.”