WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameendelea kufafanua kuhusu bei ya data za simu na kubainisha kuwa Tanzania ni moja ya nchi zenye bei nafuu zaidi ya data za simu ikiwa inashikilia nafasi ya sita kwa Afrika na nafasi ya 50 duniani.
Nape aliyasema hayo jana alipozungumza katika kipindi cha 360 kinachorushwa na televisheni ya Clouds, ikiwa ni mwendelezo wa ufafanuzi wake kuhusu bei za data aliouanza kupitia ukurasa wa Twitter hivi karibuni baada ya malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu suala hilo.
Nape alisema serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambaye ndiye mdhibiti wa mawasiliano ya simu nchini, imekuwa ikifanya udhibiti wa viwango vya bei za kusafirisha data kulingana na tathmini zinazofanyika kila baada ya miaka minne na kuweka viwango vinavyowiana na gharama za uendeshaji zinazotumiwa na watoa huduma.
“Katika kila kipindi cha miaka minne kunafanyika tathmini, mdhibiti anapitia sababu zote za kufanya mabadiliko ya bei ambazo ndiyo zinatupa gharama ya data, hizo sababu zinaweza kuwa gharama za uendeshaji, uwekezaji na kodi zetu zimekaaje, mara ya mwisho tulifanya 2018 na hii ndiyo inafanya tuseme kwamba soko halijaachwa huru tu,” alisema Nape.
Aliongeza kuwa katika udhibiti huo mdhibiti anaweka viwango vya juu na vya chini vya bei ya kusafirisha data kwa kipindi cha miaka minne ingawa kila mwaka kunafanyika mapitio kuona kama kuna sababu ya kubadilisha viwango kutokana na sababu tofauti ikiwemo mabadiliko ya kodi.
Alisema katika udhibiti huo ndio uliofanya Tanzania kuwa moja ya nchi yenye gharama ndogo za bei ya kusafirisha data kwa Afrika ikitanguliwa na Algeria, Libya, Ghana, Morocco ingawa bado serikali inaangalia namna ya kudhibiti bei zaidi ili kuokoa wananchi na gharama kubwa za data.
“Hii haimaanishi kwamba kwa kuwa tuko chini kwamba tuko vizuri kwa sababu uchumi wa watu wetu haufanani, inawezekana kabisa kwamba hii bei ni ya chini kulinganisha na kwingine kwa sababu uwezo wa watu wao ni mkubwa, sisi watu wetu bado ni maskini na ndiyo maana serikali inafanya udhibiti tusipande sana. Wenzetu wameachia soko liamue sisi tukifanya hivyo watu wetu watashindwa kununua data,” alisema.
Aliwataka wananchi watambue kwamba serikali haipuuzi na haitapuuza malalamiko ya wananchi wake na itafanya kila linalowezekana kudhibiti bei za kusafirisha data na kuhakikisha huduma bora za mawasiliano ya simu.
“Ndiyo sababu kuna wakati mwaka 2019 na zaidi 2020 kulitokea shida, baadhi ya watoa huduma waliamua kushuka chini ya bei elekezi ya chini ya Sh 2.03, wakapitiliza ile bei ya chini na ni katika ushindani tu ili kuvuta wateja kutoka kwa mtoa huduma mmoja kwenda kwa mwingine na kuna watu wakaamua kupanda kupitiliza kutoka 9.5 hadi 40.41 na walioshuka walienda mpaka 0.63. Malalamiko yakaanza,” alisema Nape.
Alisema malalamiko hayo yalitokana na kubadilishwa kwa huduma watoa huduma walioshuka walizidiwa na wateja na kufanya huduma kuwa dhaifu kwa hali hiyo mamlaka ikaingilia katika kuwarudisha katika viwango elekezi.
Alisema kwa tathmini itakayofanyika mwaka huu na kwa uwekezaji mkubwa uliowekwa na serikali ni matumaini yake kwamba gharama zilizobaki ni za uendeshaji na serikali inajipanga kupitia upya maeneo ya tathmini yanayoamua bei za kusafirisha data na kuona namna ya kuyafanyia kazi ili kupunguza mzigo wa gharama kwa wananchi.
Aidha, aliwataka wananchi kujifunza namna nzuri ya matumizi ya intaneti kwa kuepuka kuacha aplikesheni wasizozitumia wazi ili kuepuka kumalizika kwa vifurushi haraka na kuondoa malalamiko kuwa watoa huduma wamekuwa wakiwaibia vifurushi
Comments are closed.