Nape: Tumieni Tehama kujiingizia kipato

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewataka vijana kuitumia teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) kujiingizia kipato, badala ya  kuitumia kwa utapeli na kufuatilia umbea kwenye mitandao ya kijamii.

Alitoa kauli hiyo jana wakati akizindua minara 6 ya Kampuni ya Simu nchini (TTCL), Kijiji cha Kamalampaka kilichopo Kata ya Inyonga, wilayani Mlele mkoani Katavi.

“Tanzania tunapenda umbea saana, sasa mawasiliano haya wakati mwingine yanatumika kutafuta umbea, pamoja na umbea ili ucheke na maisha yako yaongezeke, lakini tumia kutafuta mambo yatakayoleta pesa kwenye mfuko wako.

“Tutumie vizuri, tusitumie mawasiliano vibaya kwa kutapeli watu, kuibia watu, kudanganya watu, kudanganya vitoto vya shule na mambo mengine msiende huko, tumieni kwa maendeleo,” alisema Waziri Nape.

Awali Mtendaji mkuu wa mfuko wa mawasiliano kwa wote (UCSAF), Justina Mashiba alisema mfuko huo kwa kushirikiana na watoa huduma za mawasiliano umesaini mikataba ya ujenzi wa minara 1,242 nchini, ambapo kati ya hiyo minara 1,087 tayari inafanya kazi na minara 155 iko hatua mbalimbali za utekelezaji.

Amesema endapo minara yote hiyo itakamilika itakuwa na uwezo wa kuwafikia na kuwahudumia Watanzania wapatao milioni 15.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mhandisi Peter Ulanga amesema mradi wa kuboresha mawasiliano awamu ya 5 umegharimu Sh bilioni 11.47, ambapo kati ya hizo TTCL imetoa shilingi bilioni 6.35 na mfuko wa maendeleo kwa wote nchini (UCSAF) umetoa Sh bilioni 5.15

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button