Nape: Utashi wa Samia umekuza mawasiliano

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema utashi wa kisiasa wa Rais Samia Suluhu Hassan umewezesha kuboresha sekta ya mawasiliano.

Aliyasema hayo Dodoma jana wakati wa ufunguzi wa ofisi za Makao Makuu ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano.

Alimshukuru Rais Samia na akasema bila utashi wa kisiasa sekta ya mawasiliano isingepata mafanikio hayo na watahakikisha hakuna Mtanzania anayeachwa.

Nape alisema bila UCSAF kutenga fedha na kuwezesha mawasiliano vijijini ambako hakuna mvuto wa kibiashara kampuni za simu zisingepeleka huduma na hali ingekuwa mbaya kwa wananchi wa vijijini.

Alisema uwekezaji umesaidia kufikisha mawasiliano kwa takribani asilimia 98 na kuwa hatua ya Rais Samia kuzindua ujenzi wa minara 758 ina maana Watanzania milioni 8 wataunganishwa na huduma za
mawasiliano.

“Bila UCSAF hawa watu wangeachwa nje ya mfumo jumuishi wa kifedha, leo naweza kutuma fedha kwa bibi yangu kijijini akapokea kwenye simu yake ni kwa sababu ya kazi nzuri iliyofanywa na UCSAF,” alisema Nape na kubainisha kuwa sekta ya mawasiliano nchini inakua, iko salama na inachangia uchumi wa nchi.

 

Aliongeza: “Sekta ya habari iko salama, sekta ya Tehama kwa maana ya mitandaoni kuko salama, ziko kelele za hapa na pale lakini tunadhibiti mambo yanakwenda salama ili tuhakikishe kila mtu anayetumia huduma anakuwa salama na maisha yanakwenda na mchango wake kwa uchumi unaendelea kupatikana”.

Alisema mwaka 2020 laini za simu zilikuwa milioni 51 na takwimu zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonesha kwa sasa ziko milioni 72 huku simu zenye akaunti za miamala ya fedha zilikuwa milioni 32 na sasa zimefikia milioni 53.

“Maana yake ni kwamba wale watu ambao walikuwa wameachwa nje na mfumo wa kibenki wasingekuwa sawa sawa kama tusingewaingiza kupitia huduma za mawasiliano,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button