Nape: Wananchi wakopeshwe simu kukuza uchumi

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amezitaka kampuni za simu za mkononi nchini kuwa na utaratibu wa kukopesha wananchi simu za kisasa kwa bei rahisi ili kuchochea ukuaji wa uchumi.

Alisema serikali inataka kupitia utaratibu huo ili kila mwananchi amiliki simu hizo badala ya kuendelea kutumia simu za ‘vitochi’.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Katuka kilichopo Kata ya Msanzi wilayani hapa jana baada ya uzinduzi wa mnara wa simu wenye teknolojia ya 3G+, alisema utaratibu huo utaleta mapinduzi ya mawasiliano nchini kwa kila mwananchi kumiliki simu za kisasa na hivyo kukuza uchumi.

“Kampuni hizo za simu zinaweza kuanza na wananchi wachache kwa majaribio…. lakini niwatahadharishe na nyie wananchi muwe wastaarabu mlipe. Watakaofanya ujanjaujanja wa kukwepa kulipa simu zao zitafungiwa na kuwa ‘toys’,” alisema.

Kwa mujibu wa Nape, minara ya simu 25 itajengwa ambapo vijiji 125 vitaunganishwa na mawasiliano ya simu kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 3.8 itakayosogeza huduma za mawasiliano ya simu kwa wakazi wa vijiji hivyo vilivyopo mkoani Rukwa.

“Minara 17 ya simu inaendelea kujengwa mkoani Rukwa na kati ya hiyo, saba itajengwa katika Wilaya ya Kalambo,” alisema.

Akizungumzia miradi iliyotekelezwa, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashiba, alisema lengo ni kujenga minara ya simu 1,245 ambapo minara 1,087 imekamilika kwa gharama ya Sh bilioni 150.

Aliongeza kuwa, UCSAF imeshirikiana na Kampuni ya Tigo kujenga mnara wa simu katika Kijiji cha Katuka ambapo Serikali imetoa ruzuku ya Sh milioni 112.7.

Kwa mujibu wa Mashiba, UCSAF pia umeziwezesha shule 25 mkoani Rukwa kwa vifaa vya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama). Awali, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Queen Sendiga alimweleza Waziri Nape kuwa mwambao wa Ziwa Tanganyika una changamoto kubwa ya kukosa mawasiliano ya simu na redio.

Alisema hali hiyo inawalazimu wakazi wake kupata huduma hizo kutoka nchi jirani.

Aliwataka wakazi wa maeneo ambayo minara ya simu imesimikwa kuilinda kwa kuwa ni mali yao.

Habari Zifananazo

Back to top button