NBC kushirikiana na Kano kukopesha pembejeo wakulima

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imetia saini mkataba wa maridhiano na Kampuni ya Kano Equipment ili kutoa mikopo nafuu ya kuwezesha wakulima kununua pembejeo za kilimo kwa wakati ili kuongeza tija na ufanisi katika sekta hiyo.

Makubaliano kati ya Benki ya NBC na Kano ni uungaji mkono juhudi za serikali  za kuwezesha kilimo biashara na hivyo kunyanyua uchumi wa wakulima na taifa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara, Elvis Nduguru alisema: “Sisi Benki ya NBC tukiwa wadau wakubwa wa kilimo nchini tunathamini na kutambua mchango wa kilimo katika pato la taifa. Tumejiunga na wenzetu wa Kano, ambao ni wataalamu katika masuala ya uuzaji wa vifaa vya kilimo kutoa mikopo nafuu ili kuongeza ufanisi katika uzalishaji.”

Kilimo kinachangia zaidi ya asilimia 65 ya uzalishaji nchini na kinatoa zaidi asilimia 75 ya ajira zote. Hivi karibuni Waziri wa Kilimo ametangaza mpango maalumu wa kuboresha kilimo ujulikanao kama “ajenda 10/30” ambao unalenga kuongeza ukuaji wa sekta ya kilimo kutoka asilimia 5 mpaka 10 ifikapo mwaka 2030.

Nduguru alisema kupitia maridhiano, wanunuzi wa pembejeo za kilimo kupitia Kampuni ya Kanu nchi nzima, ikiwemo matrekta, wataweza kupata mikopo nafuu na ya haraka kununua vifaa kama matrekta ndani ya siku 14.

Awali Mkuu wa Kitengo cha Kilimo wa benki hiyo, Raymond Urassa alisema makubaliano hayo yatawawezesha wakulima na wafanyabiashara waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo, kupata zana za kilimo na pembejeo kwa gharama nafuu na kwa wakati stahiki huku dhamana ikiwa ni chombo chenyewe.

Mwakilishi wa Kampuni ya Kanu Equipment, Edson Nalogwa alisema Benki ya NBC ni sehemu sahihi katika ukuzaji wa kilimo nchini ikiwa wana bidhaa mbalimbali za kusaidia kukuza kilimo.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button