NBC, wadau waendesha kliniki ya michezo kwa watoto

DAR ES SALAAM: Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), mdhamini Mkuu wa Ligi ya Kuu ya Tanzania Bara (NBC Premiere League) imeendesha msimu wa pili wa program yake ya michezo kwa watoto inayofahamika kama NBC Chanua Account Football Clinic inayolenga kuibua vipaji sambamba na kuhamasisha wazazi kuweka akiba kwa ajili ya watoto wao. Hatua hiyo ni muendelezo wa mkakati wa benki hiyo katika kukuza sekta ya michezo nchini kupitia vipaji sambamba kutoa huduma jumuishi za kifedha kwa makundi yote wakiwemo watoto.

Katika kufanikisha program hiyo iliyofanyika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam Jumapili asubuhi, benki hiyo ilihusisha wadau mbalimbali wakiwemo baadhi ya wazazi na watoto wao walioungana na baadhi ya wachezaji vinara kutoka klabu ya soka ya Simba SC wakiwemo Shomari Kapombe, Mzamiru Yassin, Ladaki Chasambi na Golikipa Hussein Abel.

Pia walikuwepo baadhi ya wachezaji wa timu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars, Stumai Abdallah na Fatuma Issa. Kupitia program hiyo benki hiyo pia ilikabidhi zawadi mbali kwa washiriki ikiwemo jezi za ushiriki pamoja na mipira. Aidha ilishuhudiwa watoto hao wakipata wasaa kushiriki programu mbalimbali za kimichezo chini ya usimamizi wa wachezaji hao wanaofanya vizuri kwenye sekta ya michezo hapa nchini ili kuwafundisha mbinu mbalimbali za kimichezo.

Akizungumzia programu hiyo iliyohusisha pia elimu kwa wazazi kuhusu fedha, umuhimu wa kuwawekea akiba watoto na malezi yenye kutoa kipaumbele kwenye michezo na vipaji vya watoto, Meneja Masoko wa NBC Alina Kimaryo alisema kupitia program hiyo inayotarajiwa kufanyika angalau mara tatu kwa mwaka, walengwa ni watoto wenye umri kuanzia miaka sita hadi kumi na tatu sambamba na wazazi au walezi wao.

”Benki ya NBC tunaamini katika imani kwamba kesho nzuri inaandaliwa leo. Kupitia program hii ya Kliniki ya mchezo ya Chanua Akaunti tunaandaa kesho nzuri kwa watoto kupitia vipaji vyao hususani vya kimichezo kwa kuzingatia ukweli kwamba michezo ni ajira. Pia tunaandaa kesho ya Watoto kupitia kuhamasisha wazazi wajenge utamaduni wa kuweka akiba kwa ajili ya Watoto wao na hiyo ndio sababu hapa unaona kuna vyote viwili yaani michezo na elimu ya fedha na akiba kwa wazazi,’’ alisema Alina.

Akizungumzia elimu ya fedha na malezi ya watoto, Msimamizi wa Huduma za Elimu wa Benki ya NBC, Yoabu Ndanzi alisema pamoja na kuwajengea uwezo na maarifa wazazi kuhusiana na umuhimu wa kuwawekea akiba watoto wao pia inalenga kuwajengea uwezo wa kutambua umuhimu wa michezo na vipaji walivyonavyo Watoto wao ili waviheshimu na zaidi waone namna ya kuviendeleza.

‘Tunashukuru kuona kwamba wazazi wengi kwenye darasa hili tayari wana uelewa wa kutosha kuhusu kuweka akiba ndio maana tayari wameshafungua akaunti za chanua kwa ajili ya Watoto wao. Tunajitahidi zaidi kuwaelewesha kuhusu kutambua umuhimu wa michezo na vipaji vya watoto wao kwa kuzingatia ukweli kwamba michezo ni ajira. Ili kuwahamasisha wazazi na watoto wenyewe tumewaletea wachezaji mashuhuri kutoka vilabu vyao pendwa vinavyoshiriki ligi kuu. Tulianza na wachezaji wa Azam FC, leo tumewaleta wa Simba SC na tukio lijali tutawaleta wachezaji wa Yanga SC wakifuatiwa na wachezaji wat imu nyingine pia,’’ alisema.

Wakizungumzia hatua hiyo wachezaji walioshiriki programu hiyo, pamoja na kuipongeza benki ya NBC kwa jitihada zake katika kuendeleza mchezo wa soka hapa nchini, walionyesha kufurahishwa zaidi na mpango huo kwa kuwa unatoa fursa kwao kushirikiana na jamii hususani watoto, hatua ambayo itasaidia sana kuwashawishi wazidi kuupenda mchezo huo sambamba na kuongeza juhudi zaidi waweze kufanikisha ndoto zao kupitia michezo.

‘’Imekuwa ni furaha sana kwetu hii leo na kwa hili tunawapongeza sana NBC kwa kuwa kupitia program hii ya NBC Chanua Account Football Clinic wametukutanisha na watoto ambao tumeweza kucheza nao, tumewaelekeza baadhi ya mbinu chache za kimichezo na zaidi tumewahamasisha waendelee kupenda michezo sambamba na kuzingatia masomo yao kwa kuwa elimu na michezo vinaweza kabisa sambamba.’’

‘’Zaidi kwa kuwa program hii inahusisha wazazi tunaamini kabisa itasaidia kubadili mitazamo yao kuhusu suala zima la kuheshimu vipaji vya watoto wao,’’ alisema mchezaji Shomari Kapombe, beki wa timu ya Simba SC.

Kwa upande wao baadhi ya wazazi walioshiriki tukio hilo wakiwa sambamba na watoto wao akiwemo Bi Tima Mohamed na Bw Khamis Kakolwa walisema wamevutiwa zaidi na program ya NBC Chanua Account Football Clinic kwa kuwa imehusisha maeneo mengi muhimu yenye manufaa kwa watoto ikiwemo michezo, elimu ya fedha na akiba, afya na malezi ya watoto huku pia ikitoa fursa kwa wazazi na watoto kufurahia pamoja sambamba na wachezaji wanaowapenda kutoka Ligi Kuu ya NBC.

Habari Zifananazo

Back to top button