NBC yaja na ‘funga mwaka kibabe’

Katika juhudi za kukuza miamala ya papo kwa papo, salama na malipo ya bila kutumia pesa taslimu nchini, Benki ya NBC imezindua kampeni yake mpya ya kibenki ya kidijitali inayoitwa “Funga Mwaka Kibabe na NBC Bank.”

Kampeni hii inalenga kukuza matumizi ya chaneli za kidijitali mtandaoni kwa wateja wa Benki ya NBC wakati wa msimu wa sikukuu.

Mapinduzi mapya ya malipo yanayofanyika kupitia viza ( Visa) yatawahakikishia usalama wateja na urahisi zaidi wa kufanya malipo.

Kupitia kampeni hii mpya, wateja wa Benki ya NBC wanaofanya miamala kupitia njia mbadala za kidijitali za NBC Kiganjani, huduma ya benki kupitia mtandao na kupitia kadi ya NBC Debit watapata fursa ya kujishindia zawadi za pesa taslimu, simu za mkononi, luninga na mengine mengi.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kidijitali wa Benki ya NBC, Ulrik Tobias, alisema kampeni hiyo mpya inalenga kuhakikisha wateja wanaweza kupata pesa zao kwa usalama na kufanya miamala kwa urahisi, kuongeza urahisi zaidi wa huduma na kuboresha uzoefu kwa wateja.

“Tunataka kuwapa wateja wetu muda wa kutosha kwa ajili ya familia na wapendwa wetu katika msimu huu wa sikukuu kwa kuwahakikishia kwamba wanaweza kufanya miamala yote ya benki wakiwa katika hali ya starehe wakiwa majumbani mwao.

“Tunaelewa kuwa wengi watakuwa likizoni na pengine kujiingiza katika matembezi mengi ya matumizi katika wakati huu. Benki ya NBC imehakikisha kuwa unaweza kufanya miamala kwa urahisi na kwa ufanisi ukiwa nyumbani huku ukipata nafasi ya kujishindia zawadi,” amesema Ulrik.

Aliongeza kuwa kampeni hiyo inalenga kuwazawadia watumiaji kwa kadiri wanavyofanya  miamala mingi, ndivyo unavyojishindia na kupokea zawadi za kampeni kama vile simu za mkononi, luninga, punguzo la asilimia 40 kwa ununuzi mbalimbali, zawadi za pesa taslimu na vocha za kufanyia manunuzi.

“Wateja wote wanaotumia kadi zetu za benki za visa, ATM, App ya NBC ya simu, na huduma za NBC Kiganjani watakuwa na nafasi sawa za kushinda zawadi hizi. Wanachotakiwa kufanya ni kufanya miamala. Kutakuwa na droo za kila wiki, droo za kila mwezi, na zawadi za papo hapo zitashindaniwa. Tunalenga kuwazawadia zaidi ya wateja 400 waaminifu. Tutahakikisha kuwa kuna miamala isiyo na matatizo katika msimu huu wa sikukuu ili wateja wetu waweze kufurahia na kupata nafasi ya kujishindia zawadi mbalimbali kwa kutumia chaneli za kibenki za kidijitali.” Alisema Ulrik.

Kampeni hiyo imeanza Desemba 2 na itadumu hadi Desemba 26, mwakani.

Benki imeshirikiana na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) ili kuhakikisha kwamba ushindi wote ni wa haki na wa wazi. Washindi watatangazwa na kutunukiwa hadharani.

Habari Zifananazo

Back to top button