Serikali imepokea kiasi cha Shilingi bilioni sita kutoka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).
Kiasi hicho ni sehemu ya gawio la kiasi cha Sh bilioni 20 ambayo NBC imetenga kwa ajili ya wanahisa wake kufuatia faida iliyopata katika kipindi cha mwaka 2022.
Serikali inamiliki asilimia 30 ya hisa za benki hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi amekabidhi gawio hilo kwa Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu aliyewakilisha Serikali katika hafla fupi ya makabidhiano hayo iliyofanyika mapema leo Jumatano, jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo limehudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka serikalini na maofisa waandamizi wa benki hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mchechu ameipongeza NBC kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika kipindi cha mwaka 2022 wakati akiwasilisha salamu za Rais Samia Suluhu Hassan.
Aliipongeza benki hiyo huku akitoa wito kwa taasisi na mashirika yenye umiliki wa umma kuhakikisha yanatimiza wajibu wao wa kuwasilisha gawio litokano na faida za uendeshaji wa shughuli zao kwa serikali.
“Serikali inafurahishwa na utendaji ulioimarika wa Benki ya NBC. Sisi kama wanahisa, tunafurahi kuona uwekezaji wetu unatoa matunda. Gawio la Sh bilioni 6 ambalo Serikali ilipokea leo litaongeza ukubwa wa kapu letu la makusanyo ambayo yamekuwa yakielekezwa katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo hususani ile ya kimkakati.
“Hivyo naipongeza sana Benki ya NBC kwa mafanikio haya…hongereni sana,” amesema Mchechu.
Mchechu ametumia fursa hiyo kusitiza agizo la Rais Samia linalotaka mashirika na taasisi nyingine zenye umiliki wa umma kuhakikisha zinatimiza wajibu wao wa msingi wa kuwasilisha gawio kwa serikali.
“Anachosisitiza Mheshimiwa Rais kwenye hili ni kwa taasisi hizi kutimiza wajibu huu kwa fedha zitokanazo na faida iliyopatikana tu na si kwa taasisi hizi kukopa mahali popote ili kulipa gawio.
“Hata hivyo taasisi zitakazoshindwa kutimiza wajibu ipo haja ya viongozi wa taasisi hizi kujitafakari ili kuona kama kweli wanastahili kuendelea kuongoza taasisi zisizo tengeneza faida kwa taifa,’’ amesema.
Akizungumza kwenye tukio hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NBC, Dk. Elirehema Doriye, alieleza kuwa mafanikio na mwenendo chanya wa benki hiyo hatua hiyo ni uthibitisho wa imani kubwa waliyonayo wateja kwa kwa Benki hiyo.
“Tuna furaha kusalia katika dhamira yetu ya kufikia malengo yetu muhimu katika kupanua nyayo zetu na kuwekeza katika teknolojia ili kuboresha uzoefu wa wateja wetu.
“Faida yetu ya kabla ya kodi ilikuwa kwa asilimia 36 hadi Sh bilioni 81.9 kutoka Sh bilioni 60 bilioni Desemba 2021,” Mwenyekiti huyo amesema.
Ameongeza kuwa: “Ongezeko hili la faida ndilo linatuwezesha kutoa Sh bilioni 20 kama gawio kwa wanahisa wetu; leo, tunafurahi kukabidhi hundi ya Sh bilioni 6 kama gawio kwa mwaka 2022. Tunatazamia mustakabali wenye matumaini zaidi huku pia tukiwa tunaendelea kutoa huduma bora zaidi kwa wateja wetu.” Alisema Bw Doriye.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi aliishukuru Serikali kwa kuweka mazingira mazuri kwa taasisi za fedha kama Benki ya NBC kustawi huku pia akiipongeza Bodi ya wakurugenzi wa benki hiyo pamoja na wafanyakazi kwa jitihada kubwa walioifanya hadi kufikia mafanikio hayo.
“Utendaji kazi wa Benki unaonyesha mazingira bora ya biashara ambayo yalituruhusu kuwafikia wateja wetu kwa urahisi. Tutaendelea kuwekeza katika teknolojia, kupanua nyayo zetu na kuboresha huduma zetu zetu ili kukidhi na kuzidi matarajio ya wateja wetu,” amesema Sabi.
Akizungumzia uwajibikaji wa benki hiyo kwa jamii Sabi amesema katika kipindi cha mwaka 2022, benki hiyo ilifanikiwa kukusanya kiasi cha Sh milioni 200 kupitia mbio za NBC Dodoma Marathon 2022 ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi.
“Benki ya NBC ndiyo mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania ‘NBC Premier League”, ambayo inazalisha ajira na kusaidia uwezeshaji na ushirikishwaji wa kifedha,” ameeleza.