NBC yapiga jeki huduma Hospitali ya Mpitimbi

SONGEA, RUVUMA: BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imetoa misaada ya vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 11.5 kusaidia kuboresha huduma za afya katika Hospitali ya Mpitimbi, Songea mkoani Ruvuma.

Vifaa hivyo ni kitanda cha kujifungulia kimoja, vitanda vya wagonjwa 15, magodoro 15, dawa na vifaa tiba.

Vifaa tiba hivyo vimekabidhiwa leo kwa Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo, Gilbert Simya aliyepokea msaada huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.

Hafla ya makabidhiano hayo ilifanyika hospitalini hapo ikihusisha viongozi waandamizi wa mkoa na hospitali hiyo akiwemo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Songea, Elizabeth Gumbo na Padri wa Jimbo Kuu la Katoliki la Songea, Wilhem Soni.

Akizungumza wakati akikabidhi msaada huo, Mkurugenzi wa Idara ya wateja wadogo na wakubwa wa NBC, Elibariki Masuke amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za benki hiyo katika kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha sekta ya afya nchini huku pia ikiwajibika kupitia sera yake ya kusaidia jamii hususani kwenye suala zima la kuboresha afya ya jamii.

Masuke alitaja baadhi ya jitihada zinazofanywa na benki hiyo katika kuboresha sekta ya afya nchini kuwa ni pamoja na mbio za NBC dodoma Marathon ambapo benki hiyo hukusanya fedha kwa ajili ya mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake nchini.

“Kupitia mbio hizi tumeweza kuleta hamasa kwa wanawake 23,000 amabao kati yao zaidi ya 1,090 wamekutwa na vimelea vya kansa hiyo na wameshapatiwa matibabu,’’

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Simya ameishukuru benki ya NBC kwa msaada huo huku akielezea namna msaada huo utakavyosaidia kuboresha huduma ya afya hospitalini hapo kutokana na wingi wa wagonjwa wanaofika kupata huduma hospitalini hapo.

Kwa upande wake Padri Wilhem Soni ameishukuru NBC kwa msaada huo akibainisha kuwa hospitali hiyo imekuwa ikipokea wagonjwa wengi wakiwemo wale wanaohitaji huduma ya kulazwa pamoja na huduma ya uzazi, hivyo msaada wa vitanda hivyo pamoja na vifaa tiba vingine vitasaidia kwa kiasi kikubwa kuwahudumia wagonjwa hao.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button