RAIS Samia Suluhu Hassan amezipongeza taasisi za fedha nchini ikiwemo Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa namna zinavyoendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kujenga mfumo jumuishi wa fedha.
Aidha ameonesha kuguswa na jitihada za taasisi hizo katika uwezeshaji wa jamii kiuchumi hususani makundi ya wanawake na vijana.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo la ofisi ya Chama cha Kuweka na Kukopa(Saccos) ya Kizimkazi Mkunguni, Mkoa wa Kusini, Unguja iliyoenda sambamba na upokeaji wa samani mbalimbali zilizotolewa na NBC kwa ajili ya saccos hiyo, Rais Samia alionesha kuguswa na namna taasisi za kifedha zinavyotumia vema sehemu ya mapato yao kurejesha kwa jamii kupitia misaada mbalimbali.
“Naamini kupitia Saccos hii ya Kizimkazi wananchi wengi wa eneo hili watafikiwa na huduma muhimu za kifedha na hivyo kuleta ukombozi wa kiuchumi kwa kaya nyingi za eneo hili. Nitoe shukrani zangu za dhati kwa Benki ya NBC kwa namna ilivyoguswa na jitihada za wakazi hawa wa Kizimkazi na hivyo kuamua kuwaunga mkono kwa kuwapatia msaada wa samani za ndani ikiwemo viti na meza kwa ajili ya ofisi yao…hongereni sana NBC,’’ alisema.
Rais Samia alitoa wito kwa wananchi kutumia vema ushirikiano unaotolewa na taasisi hizo katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, afya, michezo na kiuchumi ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Theobald Sabi alisema msaada huo ni mwendelezo wa jitihada za benki hiyo katika kuunga mkono jitihada za serikali katika kujenga mfumo jumuishi wa fedha na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
Alisema si mara ya kwanza kwa benki hiyo kushirikiana na wakazi wa Kizimkazi katika miradi ya maendeleo huku akitolea mfano wa ujenzi wa madarasa kwa ajili ya Shule ya Awali ya Kizimkazi-Mkunguni ulioambatana na utoaji wa msaada wa gari maalumu la tiba inayotoa bure huduma kwa ajili ya Mama na Mtoto kwa maeneo mbalimbali visiwani Zanzibar.
Awali akitoa taarifa fupi kuhusu Saccos hiyo, Mratibu wa Saccos ya Kimzikazi, Said Ramadhani Mgeni alisema licha ya ujenzi wa jengo hilo kuanza mwaka 2015 ulikwama kuendelea kutokana na kukosekana kwa fedha hadi pale Rais Samia ambae pia ni Mwanachama wa Saccos hiyo aliposaidia juhudi hizo kwa kuchangia Sh milioni 55 iliyosaidia kukamilisha mradi huo.