NBS kuachia takwimu za vitongoji Machi

OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeeleza kufikia mwezi Machi mwaka huu taarifa za vitongoji na vijiji zitatolewa rasmi huku akiwataka watendaji kuzitumia takwimu hizo ambazo zimetoa mwelekeo katika kutekeleza miradi pale penye upungufu.

Hayo yamesemwa Februari 13, 2024 na Meneja Idara ya Mifumo ya Takwimu za Kijiografia Benedict Mugambi alipomwakilisha mkuu wa takwimu nchini wakati akitoa mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi kwa viongozi wa makundi mbalimbali wilayani Kishapu mkoani Shinyanga

Mugambi alisema tayari zimetolewa takwimu za mgawanyo wa idadi ya watu,idadi ya kaya na taarifa zimekuwa zikitolewa awamu kwa awamu na matokeo hayo yametolewa kuanzia ngazi ya taifa hadi ya kata.

“Sisi tumekuja kuwaonyesha picha halisi ilivyokwenye maeneo yenu na sasa hivi tunaendelea na mchakato wa taarifa za kaya kwenye vitongoji na vijiji mbazo tutazitoa mwezi Machi mwaka huu”alisema Mugambi.

Mugambi alisema takwimu zinazoendelea kutokea zina mhusu kila mtu na kama watendaji wa vijiji na kata wakipewa elimu ya kutambua matokeo na maeneo yao halisi watapata wepesi wa kufahamu changamoto zilizopo na kufanyiwa kazi.

Ofisa kutoka ofisi ya takwimu Dk Mwinyi Omary akisoma taarifa za matokeo ya sensa alisema wilaya ya Kishapu ina idadi ya watu 333,483 ambapo imeonekana pia kuongoza kwa idadi ya wazee kwa mkoa wa Shinyanga.

“Watu wanaopata maji katika vyanzo vya maji vyenye visima vilivyoboreshwa ni asilimia 70 huku wanaotumia vyoo visivyo boreshwa ni asilimia 48.6”alisema Dk Omary.

Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude akiwa mgeni rasmi kwa kufungua mafunzo hayo alisema matokeo ya sensa ya watu na makazi yamemfurahisha kwani atapata kuelewa uwajibikaji wa watendaji kwenye maeneo yao kupitia ramani iliyopo.

Diwani wa kata ya Sekebugoro Frednand Mpogomi alisema kata hiyo imeonekana kuongoza kwa idadi ya watu hivyo ni fursa sasa kwa halmashauri kuipa kipaumbele katika upangaji wa bajeti kupata huduma za kijamii.

Habari Zifananazo

Back to top button