NBS yaeleza bajeti yake ya sensa

Dk Albina Chuwa

MTAKWIMU Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa amesema Bajeti ya Sensa iliyopitishwa na Bunge la Bajeti 2022/23 ni Sh bilioni 400.

Mtakwimu alitoa takwimu hizo wakati akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma Jumatano na kusema takwimu zinazosambaa mitandaoni si sahihi.

“Kiwango hicho cha fedha ni wastani wa Sh 6,265 sawa na dola 2.7 zilizolenga kuhesabu watu milioni 64,” alisema.

Advertisement

Dk Chuwa alisema fedha zote hizo zimetolewa na Hazina kutoka katika Mfuko Mkuu wa Serikali, wafadhili mbalimbali waliojitokeza walichangia katika kujengea uwezo wataalamu pamoja na kutoa vifaa vikiwemo vishikwambi.

Alisema tathmini iliyofanywa na Kamisheni ya Uchumi wa Afrika (UNECA) inaonesha kuwa kwa nchi za Afrika katika mizunguko ya miaka 2020 ni kati ya dola 2.0 hadi dola 5.0 na Tanzania kama miongoni mwake ni dola 2.7 kwa mtu mmoja.

Hata nchi jirani ya Kenya iliyofanya sensa mwaka 2019, gharama iliyotumika kwa mtu mmoja ni sawa na Sh 8,150 sawa na dola 3.52 za Kimarekani.

Sensa ya majengo iliyoanza juzi Agosti 30, mwaka huu hadi asubuhi ya Agosti 31, mwaka huu, jumla ya majengo 6,351,927 sawa na asilimia 50 yamekwishahesabiwa. Asilimia 50 zilizobaki zitakamilishwa ndani ya siku mbili hadi Septemba mosi litakapofungwa zoezi hilo.

Katika sensa hiyo ya majengo, ya kwanza ya aina yake kufanyika nchini, makarani wanakusanya taarifa mbalimbali zikiwemo za umiliki, mahali majengo yalipo na taarifa nyingine zilizoainishwa katika dodoso la majengo la maswali 27.

Hadi jana asubuhi Agosti 31, kiwango cha watu waliohesabiwa nchi nzima kimefikia asilimia 99.93 na zimebaki asilimia 0.07 ya kaya zote nchini.