Nchi 11 zakutana Dar mikakati ya uzalishaji
NCHI 11 zinakutana jijini Dar es Salaam kujadili mikakati imara inayotekelezwa kupitia sera mbalimbali za kisekta za uzalishaji, ili zizalishe kwa ubora na tija katika maendeleo ya nchi hizo.
Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, amesema hayo jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa warsha ya kujadili mikakati imara katika nchi hizo.
Kigahe amesema moja ya changamoto iliyopo nchini ni sera kupitwa na wakati, hivyo wizara hiyo inapambana, ili ziweze kuhuishwa, iwe rahisi katika utekelezaji wake.
Amesema sera nyingi katika sekta tofauti zilikuwa hazisomani, hivyo wanaangalia kama ni sekta ya nishati, madini, maji na nyinginezo ni namna gani zitasomana, ili kuhakikisha malengo ya taifa yanatimia.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti na Kupunguza Umaskini Tanzania (Repoa), Dk Donald Mmari, amesema utafiti walioufanya umejikita katika kuangalia changamoto zinazokabili sekta ya uzalishaji, hususan sekta ya viwanda.
“Tuliangalia sekta ya mafuta ya kula, nguo, sukari na uzalishaji wa bidhaa za ujenzi. Utafiti umejikita zaidi katika maeneo hayo ya kisera na mradi ulipoanza tulienda kwenye baadhi ya viwanda kwenye sekta ambazo serikali iliainisha,
“Tunapata changamoto mbalimbali sera na mikakati itafanyiwa mapitio kusudi maeneo hayo yaweze kufanyiwa kazi,” amesema.