Nchi 20 zajadili mabadiliko ya tabianchi Dar

NCHI zaidi ya 20 na mashirika ya kimataifa yamekutana Dar es Salaam kujadili ajenda za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akifungua mkutano huo Alhamis Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo alisema mkutano huo wa ngazi ya mawaziri unazikutanisha zaidi ya nchi 20 na wadau wa maendeleo wa kimataifa kujadili ajenda zitakazojadiliwa katika mikutano miwili ya mazingira baadaye mwaka huu.

Dk Jafo alisema dunia inakabiliwa na janga la mabadiliko ya tabianchi na athari zake zimeshaanza kuonekana na Tanzania zimo ikiwemo ukame uliosababisha mataifa mengi kukumbwa na njaa, kina cha maji ya bahari kuongezeka, uwepo wa viumbe vamizi na athari nyingine.

“Kikao hiki cha siku mbili kinawakutanisha wadau barani Afrika kubadilishana mawazo ya kupanga mikakati ya jinsi gani ya kuenenda kwenye mikutano hiyo miwili ya mabadiliko ya tabianchi itakayofanywa baadaye katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Tushukuru katika nchi yetu tulijiwekea malengo ifikapo mwaka 2030 tuwe tumepunguza hewa zinazoharibu anga kwa asilimia 30 hadi 40,” alisema.

Alisema serikali imeanza utekelezaji kwa kuanzisha miradi mikubwa ya kimkakati kama ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) itakayounganisha Dar es Salaam na nchi jirani zisizo na bandari.

Aidha, alisema mradi mwingine wa kimkakati wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ni ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme katika Mto Rufiji litakalozalisha megawati zaidi ya 2,116.

Mradi mwingine wa kimkakati kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi alisema ni uwekezaji wa mradi wa ujenzi wa mwendo kasi katika Jiji la Dar es Salaam ambao unapunguza hewa zinazoharibu anga.

Lakini pia alisema bajeti ya mwaka huu ya Wizara ya Kilimo imeongezeka mara tatu na eneo kubwa limeelekezwa kwenye umwagiliaji kama hatua ya kukabiliana na athari za ukame.

Alisema asilimia 32 ya eneo lote la nchi limehifadhiwa lakini pia nchi ina jumla ya ukubwa wa hekta milioni 48.1 za misitu iliyohifadhiwa inayosaidia kunyonya hewa joto zinazosaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Alisema kampeni ya upandaji miti kila mwaka zinaendelea lengo likiwa ni kupanda miti milioni 276 kila mwaka.

Akizungumzia athari za mabadiliko ya tabianchi Zanzibar, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk Omar Shajak alisema visiwani humo athari hizo ni kubwa na maeneo mawili yamekumbwa zaidi.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni sekta ya kilimo na kwamba mashamba mengi ya mpunga yameathiriwa na maji ya chumvi kupanda juu na hivyo kupunguza eneo la uzalishaji chakula.

Awali, Balozi wa Uingereza nchini, David Concar, alisema ushirikiano wao na Tanznaia umewezesha kuleta mataifa hayo 20 kujadili athari za mabadiliko ya tabianchi.

Alisema malengo ni kuendelea kuhimiza njia mbalimbali kuchukuliwa ili kupunguza hewa ya ukaa.

 

Habari Zifananazo

Back to top button