DAR ES SALAAM: KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema watanzania wanapaswa kumuenzi Hayati Edward Lowassa kwa kuchapa kazi huku akinukuu salamu ya ‘Good Morning’ kama kauli aliyoipenda.
Akimuelezea Waziri Mkuu huyo wa zamani ambae anatarajiwa kuzikwa siku ya Jumamosi Monduli mkoani Arusha Nchimbi amesema “Good morning hivi ndivyo alivyotusalimu Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa kila alipoingia kwenye kikao chochote cha kikazi, iwe asubuhi iwe mchana au usiku alimradi ni kazi, salamu yake ilikuwa ‘Good morning’ alimaanisha kazi inaanza wekeni kila kitu pembeni tufanye kazi, ” amesema Nchimbi
Amesema, Lowassa, alikuwa kiongozi jasiri, mkweli, mpenda maendeleo na muumini wa kweli wa muungano na umoja wa watanzania.
“Aliheshimu watu wote bila kujali rika, nafasi au uwezo wa kifedha. Akiwa rafiki yako ni rafiki yako kweli kweli, ” amesema Nchimbi na kuongeza
” Lowassa alikuwa kaka yangu, rafiki yangu na mwalimu wangu na mtu mwenye mchango mkubwa katika safari yangu uongozi, ” amesema
Aidha amesema namna pekee kwa watanzania kumuenzi Lowassa ni kwa kuchapa kazi kwa bidii kwa sababu alikuwa mtu hodari kwa kutetea maslahi ya watu bila kujali wanakotoka, imani zao wala mrengo wao wa kisiasa.
“Tutamkumbuka kwa mchango wake katika ujenzi wa taifa letu, ” amesisitiza Nchimbi.