Nchimbi Katibu Mkuu CCM, Rais ampongeza

BALOZI Dk Emanuel Nchimbi ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akichukua mikoba ya Daniel Chongolo.

Kwa mujibu wa Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda akizungumza na HabariLEO amesema Halmashauri Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan imemteua Nchimbi leo Januari 15, 2023 Unguja, Zanzibar

Nchimbi anachukua mikoba ya Daniel Chongolo ambae alibwaga manyanga kwa kujiuzulu wadhifa huo hivi karibuni.

Chongolo alijiuzulu kwa kile alichodai ni kuchafuliwa kwenye mitandao ya kijamii na kuandika barua kwa Rais Samia ambae aliridhia ombi lake hilo la kujiuzulu.

Balozi Nchimbi ni mbobezi katika medali za siasa na diplomasia akiwa anahitimu IDM Mzumbe mwaka 1997 alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na mwaka uliofuatia (1998), alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM).

Dk Nchimbi amewahi kuajiriwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kati ya mwaka 1998 – 2003.

Alisoma shahada ya uzamili ya usimamizi wa biashara Chuo Kikuu cha Mzumbe mwaka 2001 – 2003 akibobea kwenye maeneo ya (benki na fedha).

Dk Nchimbi aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda (mwaka 2003 – 2005) na (mwaka 2008 – 2011) alisoma na kufanikiwa kuhitimu shahada ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Mzumbe.

Dk Nchimbi amemuoa Jane na wana watoto watatu.

Mbio za ubunge

Dk Nchimbi alirudi nyumbani kwao Songea Mjini kuanza harakati za ubunge tangu alipokuwa anaongoza UVCCM.

Ilipotimu mwaka 2005, aliingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi akakutana na Edson Mbogoro wa Chadema aliyekuwa mpinzani wake mkuu. Dk Nchimbi alisaidiwa na mtandao mkubwa wa CCM na kupata ushindi wa asilimia 67.6 dhidi ya asilimia 30.5 za Mbogoro.

Mara tu baada ya kuwa mbunge, Rais Kikwete alimteua kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, hii ilikuwa Januari 2006, alidumu kwenye wizara hiyo hadi Oktoba 2006 alipohamishiwa kwenye Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana.

Pia amewahi kuwa Waziri wa Ulinzi na Kujenga Taifa hadi Novemba 2010.

Upandaji vyeo wa Nchimbi uliendelea, Rais Kikwete alimpa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo akiwa Waziri kamili, alidumu hapo hadi Mei 2012 alipohamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani kabla ya kujiuzulu Desemba 2013.

Mwaka 2017 Hayati Rais John Pombe Magufuli alimteua kuwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil na badae Rais Samia kumteua kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri kabla ya kumrudisha nyumbani hivi karibu.

Habari Zifananazo

Back to top button