Ndalichako aagiza mafunzo sekta zisizo rasmi

WAZIRI wa Nchi ,Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana , Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako ameuelekeza Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa kushirikiana na wadau wengine kuendelea kutoa mafunzo katika sekta isiyorasmi.
Ameutaka wakala huo kutenga bajeti itakayotumika katika utoaji wa mafunzo na elimu endelevu kwa kushirikiana wadau katika sekta isiyorasmi ambayo imeonesha kuadhirika zaidi ya ajali na vifo sehemu za kazi.
Profesa Ndalichako ametoa agizo hilo Aprili 28, 2023 katika kilele cha Maadhimisho ya siku ya Usalama na Afya Duniani ambayo kitaifa imefanyika mkoani Morogoro.
Waziri Profesa Ndalichako amesema kwa bahati mbaya katika sekta isiyo rasmi wanafanya kazi katika mazingira magumu na mara nyingi hata huduma za ukaguzi mahala pa kazi haziwafikii kwa kiwango kinachotakiwa .
Profesa Ndalichako amesema kwa sasa hakuna mfumo ambao ni rasmi uliaondaliwa kuripoti ajali na magonjwa yanayotokea katika sekta isiyorasmi ,na hivyo ina kuwa ni vigumu kufahamu takwimu kwa uhakika na hali halisi ya usalama na afya katika sekta hiyo.
“ Nichukue nafasi hii katika maadhimisho haya ya Usalama na Afya Duniani kuwaelekeza Osha kwa kushirikiana na wadau wengine kuendelea kutoa mafunzo katika sekta hii isiyorasmi” amesema Profesa Ndalichako
Waziri hiyo amesema kuwa mafunzo hayo yawe ni endelevu na sio kusubiri wakati wa maadhimisho ya siku ya Usalama na Afya Duniani na ili kufanikisha lengo hilo , Wakala huo haina budi kutenga bajeti ya kuwafikia wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi.
“ Kama mlivyofanya safari hii mmetoa mafunzo kwa Wajasiliamali 3,748, lakini iwe ni endelevu na mtenge na bajeti “ amesma Profesa Ndalichako
Waziri Profesa Ndalichako amesema , Ofisi yake isingependa kuona mfanyakazi iwe katika sekta rasmi au sekta isiyo rasmi anapata madhara anapokuwa kazini .
Profesa Ndalichako amewataka wadau kuunga mkono jitihada za Rais Dk Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akiendelea kuzalisha ajira kupitia sekta ya Umma na amekuwa akiendelea kuimarisha sekta binafsi ambayo inazalisha ajira kwa Watanzania .
“ Tumuunge mkono kwa kuhakikisha ya kwamba tunaweka amzingira ambayo yatalenga kupunguza au kundoa ajali na vifo vinavyotokana na kazi” amesema Profesa Ndalichako
Profesa Ndalichako amesema kwa pamoja kama Taifa tutaweza kuwa na suluhisho la matatizo ya usalama na afya mahali pa kazi endapo watafanya kazi kwa ushirikiano .
Hivyo amezotaka mamlaka za utatu pamoja na waajiri kuendelea kuimarisha mifumo ili kuendelea kulinda nguvu kazi ya Tanzania .
Profesa Ndalichako amesema serikali inaendelea kuthamini na kutambua juhudi za taasisi za umma na binafsi zinavyojituma katika kuboresha mazingira ya kazi na kwa wafanyakazi wao bila kushurutishwa .
“ Sheria zipo lakini tunafurahi tunapoona watu wanatii sheria bila shuruti “ amesema Profesa Ndalichako
Amesema serikali itaendelea kuhakikisha ya kwamba kusimamia usalama na afya mahali pa kazi na aliwakumbusha waajiri kuzingatia kauli mbiu yam waka huu “ Mazingira Salama na Afya ni Kanuni na Haki ya Msingi Mahali pa Kazi”.