Ndaruke aibuka kidedea CCM Kibiti
Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Kibiti mkoani Pwani kimepata viongozi wapya baada ya kufanyika uchaguzi wa ndani wa chama hicho hapo mwishoni mwa wiki huku Juma Kassim Ndaruke ameibuka mshindi.
Kada huyo ameshinda kinyang’anyiro hicho baada ya kumshinda mpinzani wake wa karibu, Abdujabiri Malombwa ambaye alikuwa akitetea nafasi hiyo kwa mara ya tatu.
Kwenye nafasi hiyo ambayo wagombea walikuwa watatu, Ndaruke alishinda kwa kupata kura 428 dhidi ya 385 za Malombwa huku mgombea wa tatu Abdallah Mpili akipata kura saba pekee.
Ushindi wa Ndaruke unamaanisha kuwa mwanasiasa atakuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibiti kwa miaka mitano ijayo (2022-2027).
Akizungumza na Wajumbe wa Mkutano wa chama hicho ngazi ya wilaya, Mwenyekiti huyo mteule Ndaruke alisema kuwa ni fahari kuona wajumbe wakuwapa nafasi za uongozi ndani ya chama.
“Natumia fursa hii kwanza kumshukuru Mungu, wajumbe pamoja na kila mmoja wetu aliyeshiriki kwenye uchaguzi. Naomba kusema kuwa hapa aliyeshinda sio Ndaruke mbali CCM ndio imeshinda.
“Tunapokwenda kuanza kazi na uongozi upya nataka kukuchukua fursa hii niwaambie kuwa tutaenda kujenga CCM imara yenye dira na ambayo itakuwa na uwezo wa kuisimamia serikali ili kuhakikisha ya kwamba miradi ya maendeleao kwenye wilaya yetu inatekelezwa pamoja na kumalizika kwa wakati’, alisema Ndaruke ambaye pia ni Mwenyekiti wa UVCCM mstaafu wa wilaya hiyo’.
Akizungumza baada ya kukubali matokeo, mpinzani wa karibu wa Ndaruke amekiri kuwa ameshindwa kihalali kabisa. Lazima tukumbali kuwa uongozi ni kupokezana vijiti, muda wangu wa utumishi kama Mwenyekiti wa wilaya umemalizika na kwa sasa kijiti namuachia Ndugu Ndaruke’.
Walioshinda nafasi za ujumbe wa Mkutano Mkuu ngazi ya Mkoa ni Ashura Matimwa na Uwesu Mtandika huku Ally Seif, Khalid Mtalazaki na Rehema Mkumba wakishinda nafasi za ujumbe wa Mkutano Mkuu Taifa.