TOKYO, Japan: UWANJA wa Ndege wa Haneda uliopo Tokyo umekumbwa na tukio la kutisha wakati ndege ya Japan Airlines, Flight 516 ilipoanza kuwaka moto baada ya kutua.
Ndege hiyo, iliyokuwa imetoka Uwanja wa Ndege wa New Chitose karibu na Sapporo, ilibeba abiria na wafanyakazi 379. Tukio hilo lilitokea saa 11:47 jioni kwa saa za hapa, ikisababisha kufungwa kwa haraka kwa njia zote za kutua katika Uwanja wa Ndege wa Haneda.
Licha ya taswira ya kutisha ya ndege ya Japan Airlines ikiwaka moto kwenye uwanja, juhudi za haraka za kuwahamisha watu wote kwenye ndege zilifanikiwa, kama ilivyothibitishwa na taarifa kutoka Japan Airlines.
Picha na video zenye kushtua za ndege inayowaka moto zilisambaa mtandaoni, zikionesha ukali wa tukio hilo. Uchunguzi wa kina unaendelea kubaini chanzo cha moto, na ripoti za awali zinaashiria uwezekano wa kugongana na ndege ya ulinzi wa pwani ya Japan wakati wa kutua.