Ndege ya mizigo ya ATCL yaongeza safari

BAADA ya ndege mpya ya mizigo ya Tanzania aina ya Boeing 767-300F kuanza kusafirisha mizigo juzi kwenda Dubai, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Ladislaus Matindi amesema ndege hiyo pia itafanya safari kwenye nchi mbalimbali ikiwemo India.

Ameyabainisha hayo alipozungumza na HabariLEO jana.

Juzi Mkurugenzi wa Biashara wa ATCL, Patrick Ndekena alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa ratiba ya safari za ndege hiyo kwenda Dubai itakuwa mara mbili kwa wiki yaani Jumatatu na Ijumaa.

Hata hivyo, Matindi alisema ndege hiyo ya mizigo mbali na kwenda Dubai pia itakuwa inafanya safari za kusafirisha mizigo kati ya Dar es Salaam na Mumbai nchini India kila Jumatano.

Pia alisema itakuwa inafanya safari kati ya Dar es Salaam na Kinshasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kurudi Dar es Salaam kila Alhamisi, Dar es Salaam-Lubumbashi (DRC)-Dar es Salaam kila Jumamosi.

“Tunasubiri kumalizika kwa taratibu za kupewa kibali cha kuingia China na Kenya. Pia tutafanya safari za kukodi kwenda sehemu yoyote yenye mizigo,” alisema Matindi.

Aidha, kuhusu safari hiyo ya kwenda Dubai juzi, Matindi alisema ndege hiyo ilikuwa imebeba tani 28 za mzigo wa kampuni moja kwenda Falme za Kiarabu (UAE).

Alisema wakala wao aliyeko Dubai alisema kuna mzigo wa bidhaa mbalimbali ambao ndege hiyo itausafirisha kwenda Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Matindi, ndege hiyo ikitoka Dubai itapitia Zanzibar ambako kuna soko kubwa la vifaa vya umeme pamoja na simu zinazohitajika kwa wingi kwenye soko la Zanzibar na baada ya hapo itarudi Dar es Salaam.

Habari Zifananazo

Back to top button