Ndege yaanguka ziwani Bukoba

NDEGE ya Jeshi imeanguka ndani ya Ziwa Victoria mapema leo Julai 20,2023 karibu na Uwanja wa Ndege wa Bukoba.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasia Chatanda amesema ndege hiyo ya jeshi yenye namba JW 9127, imeanguka wakati marubani wake wawili walipokuwa kwenye mazoezi ya kawaida.

Amesema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa 3:30 asubuhi Julai 20, 2023 na kuibua hofu miongoni mwa wakazi wa Manispaa ya Bukoba, ambao wamerejewa na kumbukumbu ya tukio la ndege ya abiria ya Kampuni ya Precision Air kuanguka ndani ya Ziwa Victoria na kusababisha vifo vya watu 19 na majeruhi 26 mwaka jana.

Kamanda Chatanda amewataja majeruhi hao ni Leonard Nkundwa (45) na Alex Venance (30), ambapo wamepelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera kwa matibabu.

Alijuna Theobard, mkazi wa mtaa wa Nyamkazi Manispaa ya Bukoba, ambaye ni miongoni mwa mashuhuda wa ajali hiyo amesema kuwa mwanzoni alishuhudia ndege mbili ndogo zikizunguka na kuondoka katika anga la mji wa Bukoba.

‘’Tangu jana Julai 19, 2023 niliona ndege ndogo zikipita juu ya anga la mji wa Bukoba, leo asubuhi pia nimezishuhudia ndege hizo mbili zikipita angani kabla ya kusalia ndege moja, baada ya muda tukapata taarifa kuwa kuna ndege imeanguka ziwani; lakini wengine wakadai ni mazoezi ya utayari wa uokoaji wakati wa ajali,’’ amesema Theobard.

Habari Zifananazo

Back to top button