Ndejembi acharuka utekelezaji miongozo ya ujenzi

TANGA: Naibu Waziri Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Deogratius Ndejembi amewataka wahandisi na wasimamizi wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya shule, kuzingatia miongozo ya ujenzi inayotolewa na Serikali wakati wa uletaji wa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo.

Ameyasema hayo jijini Tanga wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa Shule mpya ya Msingi Jaje iliyojengwa na fedha za mradi wa uboreshaji upatikanaji wa fursa sawa katika ujifunzaji bora wa Elimu ya Awali na Msingi (BOOST), na Shule mpya ya Sekondari Magaoni iliyojengwa kwa fedha za mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP).

Naibu Waziri, Ndejembi amesema iwapo muongozo wa ujenzi umeelekeza kutumika kwa force Account, wahandisi na wasimamizi wa miradi wanatakiwa kutumia njia hiyo na si vinginevyo, na iwapo kunahitajika mabadiliko, waombe kibali TAMISEMI.

Advertisement

Amesema hatavumilia watendaji wa serikali watakao cheza na fedha za miradi, ikiwa ni pamoja na kukaa na fedha bila kutumika na kuchelewesha ukamilikaji wa mradi.

Ndejembi ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Tanga kuchunguza manunuzi ya saruji katika Shule ya Msingi Jaje, ambapo imeonyesha kununuliwa kwa bei ya juu kuliko Wilaya jirani ya Pangani iliyo mbali na kiwanda cha Saruji.

Aidha akiongea na watumishi wa Jiji la Tanga,  Ndejembi amewataka watumishi hao kutokufanya kazi kwa mazoea, na kwamba wajitume kutimiza wajibu wao ili kuisaidia halmashauri kuhudumia jamii.

 

11 comments

Comments are closed.