Ndejembi aiagiza Takukuru kufanya uchunguzi ndani ya siku 7

NAIBU  Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),  Deogratius Ndejembi amemuagiza Afisa wa TAKUKURU wilaya ya Manyoni  kufanya uchunguzi ndani ya siku saba  juu ya mapungufu yaliyobainika kwenye ujenzi wa mradi wa shule maalum ya Sayansi ya wasichana mkoani Singida.

Ndejembi amesema uchunguzi huo uwasilishwe  TAMISEMI ili hatua sitahiki zichukuliwe.

Ametoa maelekezo hayo alipofanya ziara ya kukagua shule ya Sayansi ya kidato cha kwanza hadi cha sita inayojengwa Solya wilaya ya Manyoni kwa gharama ya  shilingi bilioni 3.

Ndejembi amebaini mapungufu katika usimamizi wa ujenzi wa shule hiyo ikiwa ni pamoja na kutofuatwa mwongozo wa manunuzi na taratibu za malipo kwa Mkandarasi anayeendelea na ujenzi.

Aidha, Ndejembi amemuagiza Mkurungenzi wa halmashauri kuwachukulia hatua za kinidhamu afisa manunuzi na mhandisi kwa kufanya malipo kwa mkandarasi kinyume na taratibu ambapo malipo yalifanyika kabla ya kibali cha malipo kutolewa pomoja kununua vifaa zaidi ya BQ iliyoelekeza.

Amesema Rais, Samia Suluhu Hasaan mwezi Januari 2022 alitoa Sh bilioni 3 za awamu ya kwanza  kujenga shule hiyo ambayo ilitakiwa kukamilika mwezi Desemba 2022 na kuanza kupokea wanafunzi mwezi Januari mwaka huu lakini mpaka sasa ujenzi haujakamilika.

Mkoa wa Singida ni moja kati ya mikoa 10  nchini iliyopokea  kiasi cha shilingi Bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za wasichana za mikoa ili kujenga vyumba vya madarasa 12, jengo la utawala 1, maabara 4, maktaba 1, matundu ya vyoo 16, chumba cha Jenereta, Bwalo, Mabweni 5, Mitaro ya maji, Kichomea taka, Matanki ya chini ya maji, Matanki ya Plastiki, Uzio, njia za kutembea na nyumba mbili za walimu.

Habari Zifananazo

Back to top button