Ndugulile awania ukurugenzi Shirika la Afya Duniani
DODOMA; Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile, amejitokeza kuwania nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani kwa Kanda ya Afrika.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2024/25 mjini Dodoma leo, amesema Tanzania ni mwanachama katika taasisi, mashirika na jumuiya mbalimbali za kikanda na kimataifa na anachama huo una faida mbalimbali kwa nchi ikiwemo za kiuchumi, kiufundi na ushirikiano.
“Wizara inaboresha mkakati wa kuhakikisha Watanzania wananufaika ipasavyo na fursa za ajira na ujumbe kwenye kamati zinazosimamia mikataba ya kimataifa pamoja na kusimamisha Watanzania wenye sifa kwenye nafasi za uongozi kwenye taasisi, mashirika ya kikanda na kimataifa.
“Natoa rai kwa watanzania wote wenye sifa, wakiwemo Wabunge wa Bunge hili tukufu, kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika taasisi za kikanda na kimataifa. Na hapa napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Mhe. Dk Faustine Engelbert Ndugulile (Mb.) kwa kujitokeza kuwania nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani – Kanda ya Afrika.
“Napenda kulifahamisha Bunge lako tukufu kwamba Serikali imeridhia kumsimamisha Mhe. Ndugulile kuwa mgombea wa nchi. Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Balozi za Tanzania zilizopo ndani na nje ya Afrika zitahakikisha anapata ushindi katika uchaguzi huo,” amesema.