NEC kusaidia wenye mahitaji maalumu

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imewajengea uwezo baadhi ya watumishi wake ili kuwahudumia watu wenye mahitaji maalumu hususani viziwi.

Hatua hiyo imelenga kuhakikisha watu wenye mahitaji maalumu hususani viziwi wanashiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kikamilifu.

Akizungumza na HabariLEO wakati wa maadhimisho wa Wiki ya Sheria yanayoendelea jijini hapa, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Sheria wa NEC, Rose Chilongozi alisema hatua hiyo imetokana na kubaini kuachwa kwa baadhi ya watu wenye mahitaji maalumu.

“ Kila uchaguzi mkuu unapomalizika, Tume ni lazima ifanye ufuatiliaji na tathimini ya kina, na kupitia ufuatiliaji na tathimini hiyo tumebaini kuwa kuna kundi hatujalijumuisha kwa sababu hawajui kinachoendelea kutokana na watumishi wa Tume kutoweza kutoa elimu wakati wa uchaguzi kwasababu watumishi wetu hawajui lugha ya alama.

“ Tume kwa kushirikiana na wadu wetu tumeendesha mafunzo ya lugha ya alama kwa watumishi wetu na watumishi wawili wamepata mafunzo ya ubobezi zaidi katika eneo hilo,” alisema na kuongeza:

“ Tunaamini kwa hatua hii na kupitia watendaji wetu hawa tumetatua changamoto walizokuwa wanakutana nazo watu ambao ni wapiga kura na wagombea wa vyama vya siasa, hii inamaana sasa tutawashirikisha ipasavyo kwenye shughuli za uchaguzi.”

Naye Ofisa Elimu kutoka NEC ambaye ni mtaalamu wa lugha ya alama, Johari Mutani alisema wakati wa kuelekea katika uboreshaji na uandikishaji wa wapiga kura kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura Tume wamekuja na program maalumu ya kufikisha elimu kwa watu ambao ni viziwi na wasioona.

Alisema kupitia program hiyo, Tume itatengeneza filamu fupi fupi za lugha ya alama ambazo zitaeleza majukumu ya Tume, sifa za mpiga kura, mgombea anapaswa kuwa na sifa gani katika ngazi za urais, mbunge na diwani.

“ Tutakuwa tunatoa elimu kwa njia ya lugha ya alama kupitia filamu hizo, mfano tutakuwa tunaeleza ni sifa zipi zinamfanya mtu agombee nafasi mbalimbali za uongozi na mambo yapi yanamfanya mtu kukosa sifa za kugombea.

“ Pia kunakuwa na malalamiko, mfano mtu amejiandikisha katika Daftari la Mpigakura lakini si raia kuna taratibu za kuweka mapingamizi hivyo hata watu wenye mahitaji maalumu wana haki ya kuzijua kwa sababu wana haki ya kugombea.

Mutani aliongeza: “pia tutakuwa na vinasa sauti kwa wasioona, vitakuwa na elimu yote ya ambayo mwananchi anapaswa kujua tunataka kama kuna mtu hataweza kusoma maandishi ya kawaida, basi ataweza kupata elimu kwa njia ya sauti na kwa lugha ya alama.”

Habari Zifananazo

Back to top button