HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa (NEC) imepokea na kujadili kwa kina taarifa ya makubaliano ya uwekezaji na uendeshaji wa bandari ambapo imeazimia kuwa uwekezaji na uendeshaji wa bandari una manufaa kwa uchumi wa nchi.
Imesisitiza kuwa uwekezaji huo ni utekelezaji wa vitendo wa Ilani ya CCM ya Mwaka 2020 – 2025, ibara ya 59, ukurasa wa 92.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo Julai 9, 2023 mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema, amesema NEC imeiagiza serikali kutoa elimu zaidi kuhusu manufaa ya uwekezaji huo.
“NEC imeielekeza serikali iongeze kasi ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya uhalisia uliomo katika makubaliano ya uwekezaji na uendeshaji huo wa bandari,” Mjema alieleza.
Amesema katika kikao hicho cha kawaida kilichoongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kilitanguliwa na Kikao cha Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.
“Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa kauli moja imezipongeza serikali zote mbili za Chama Cha Mapinduzi, Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania chini ya Dk. Samia na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuendelea kutafsiri kwa vitendo llani ya CCM ya Mwaka 2020-2025, kwa maslahi na ustawi wa Watanzania wote,” alieleza.
Comments are closed.