NEC yataka weledi usimamizi wa Uchaguzi

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi wa ngazi ya jimbo na kata, kuhakikisha wanaajiri watendaji wa vituo wenye weledi,wanaojitambua na kuacha upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi.

Mjumbe wa NEC , Magdalena Rwebangira,ametoa agizo hilo Novemba 16, 2022 katika hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi, ngazi ya kata na majimbo yanayofanyika kwa muda wa siku tatu mjini Morogoro.

“Tuhakikishe tunaajiri watu wenye weledi kadri inavyowezekana tuache masuala ya kuajiri kwa upendeleo yaani ndugu na jamaa zetu ambao hawana sifa, hii itatuharibia”amesema Rwebangira

Advertisement

Rwebangira pia amewataka kufanya utambuzi wa vituo vya kupiga kura mapema ili kubaini mahitaji maalumu ya vituo husika, kwa lengo la kuhakikisha mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani .

Amesema kuwa mafunzo hayo yanatolewa baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutangaza Desemba 17, 2022 kuwa ni siku ya uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Amani Tanzania Zanzibar na udiwani katika kata 12 za Tanzania Bara.

Rwebangira amesema kata zitakazofanya uchaguzi huo na halmashauri zake katika mabano ni Njombe Mji ( halmashauri ya Mji wa Njombe) Mwamalili ( halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga ), Vibaoni (halmashauri ya Mji Handeni) , Lukozi ( halmashauri ya wilaya ya Lushoto) na Misigusugu ( halmashauri ya Mji Kibaha ).

Kata nyingine ni Dabalo ( halmashauri ya wilaya ya Chamwino ), Mndumbwe ( halmashauri ya wilaya ya Tandahimba( Majohe ( halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ) , Kalumbaleza ( halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga) Ibanda ( halmashauri ya wilaya ya Kyela ), Mnayanjani ( halmashauri ya Jiji la Tanga ) na Dunda ( halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo).

 

Rwebangira aliwataka kuvishirikisha vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi katika maeneo yao katika masuala ya kiuchaguzi ambayo wanastahili kushirikishwa kwani jambo hilo litawarahisishia utekelezaji wa majukumu yao.

Mjumbe huyo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi aliwakumbusha kuwa ,katika utendaji wa majukumu yao wanapaswa kuzingatia katiba ya nchi, sheria za uchaguzi na kanuni zake, maadili ya uchaguzi na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume hiyo.

“Baadhi yenu mnauzoefu katika uendeshaji wa uchaguzi, hakikisheni mnazingatia maelekezo ya tume badala ya kufanya kazi kwa mazoea”amesema Rwebangira.

Katika hatua nyingine amewataka siku ya uchaguzi kuweka utaratibu utakaowezesha kila kituo cha kupiga kura kinafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufanya mawasiliano na tume pale ambapo utahitajika ushauri kuhusiana na masuala ya uchaguzi.

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *