Nelson Mandela kuongeza umahiri kidijiti

Taasisi ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia Afrika (NM-AIST)

TAASISI ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia Afrika (NM-AIST) imesaini mkataba wa ujuzi wa kidijiti na Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia utoaji wa vyeti vya kompyuta (ICDL) kwa lengo la kuongeza ufanisi katika ufundishaji.

Akizungumza jana katika hafla hiyo, Makamu Mkuu wa taasisi hiyo, Profesa Emmanuel Luoga alisema Nelson Mandela imeamua kushirikiana na taasisi hiyo ili kuleta umahiri zaidi katika ufanisi wa kazi.

Alisema lengo kubwa ni kujenga uwezo wa kidijiti katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo na kielimu katika kuhakikisha sekta ya mawasiliano inakua zaidi.

Advertisement

Luoga alisema chuo hicho kitakuwa na mtandao wa mawasiliano ya teknolojia ikiwamo umahiri katika kuhakikisha masuala ya mawasiliano yanakwenda kasi kutokana na utandawazi.

“Tunataka chuo chetu kiwe cha kwanza katika umahiri wa utoaji ujuzi wa kidijitali katika masuala ya kompyuta,” alisema.

Meneja wa Kanda wa ICDL nchini, Edwin Masanta alisema wameamua kushirikiana na taasisi hiyo katika kuhakikisha wanaongeza utendaji kazi na ufanisi.

Alisema Tanzania ya viwanda ni lazima iendane na kasi ya teknolojia ya kompyuta katika kuhakikisha ubora wa maendeleo unaoendana na kasi ya ukuaji wa uchumi kwa kutumia kompyuta.

Kaimu Ofisi ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Mipango, Teknolojia na Utawala, Kelvin Mtei alisema programu hiyo ya kompyuta itawasaidia katika kuongeza tija za ufanisi katika utendaji kazi.