Newala wahamasisha kilimo cha mpunga

HALMASHAURI ya  Mji wa Newala,  Wilaya ya Newala mkoani Mtwara imeamua kuhamasisha kilimo cha mazao mbadala ikiwemo mpunga.

Akizungumza leo wilayani hapa, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Shamimu Daudi, amesema kwa muda mrefu halmashauri imekuwa ikitegemea aina moja ya mapato yake yanatokana na zao la korosho.

Amesema wameamua kubadilisha mfumo na kuhamasisha wananchi kulima kilimo cha mazao mchanganyiko.

Kufuatia jitihada hizo, halmashauri imefanikiwa kupata skimu ya Chikwedu Chipamanda iliyopo Kata ya Mcholi Moja, kwenye halmashauri hiyo ambayo imepakana na Mto Ruvuma.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Newala, Shamimu Daudi, (Picha na Sijawa Omary).

Amesema skimu hiyo itatumika  kwa ajili ya shughuli hiyo ya kilimo cha mpunga pamoja na mazao mengine licha ya kuwa halmashauri imehamasisha wakulima walime zaidi kilimo cha mpunga.

” Kama halmashauri tumehamasisha wananchi kuhusiana na kilimo mbadala na kilimo cha mpunga, sasa hivi tunavyozungumza wakulima wetu wengi wamehamasika kulima mazao mchanganyiko kama vile alizeti, mahindi, mihogo lakini sisi tunahamasisha zaidi kilimo cha mpunga,”amesema Daudi.

“Skimu ile ikitumika vizuri ina uwezo wa kutuhakikishia chakula kwa mwaka mzima wana Newala wote, hivyo tutamsaidia mkulima kuongeza kipato, kupunguza ununuzi wa vyakula,” amesema.

Amesema skimu itasaidia kuleta mzunguko wa fedha ndani ya halmashauri hiyo, lakini pia wananchi kupata uhakika wa mazao ya chakula chake na kumuwezesha kufikiri vizuri changamoto za afya hatimaye kupata maendeleo kutoka hatua moja kwenda nyingine.

 

Habari Zifananazo

Back to top button