loader
Picha

Magufuli hataki wanasiasa wazisemee taasisi za dini

RAIS John Magufuli amesisitiza kauli yake ya serikali kuendelea kushirikiana na dini zote nchini huku akiomba madhehebu yote ya dini, kuhakikisha wasemaji wao wanakuwa watu wa dini husika, ili kuepuka kutolewa kwa matamko na kauli zinazoongezwa chumvi.

Kauli hiyo aliitoa jana Dar es Salaam wakati akikagua ujenzi wa Msikiti Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), unaojengwa kwa ufadhili wa Mfalme Muhammed VI wa Morocco.

Akizungumza wakati akikagua ujenzi wa jengo hilo kubwa na la kisasa litakalokuwa na uwezo wa kuchukua waumini 8,000, Rais Magufuli alimsifu Mufti wa Tanzania, Shehe Mkuu Abubakary Zubeir kwa kufanya kazi vizuri na kusema serikali inasikiliza dini zote nchini na itaendelea kushirikiana nao.

“Nikupongeze Mufti wa Tanzania unafanya kazi vizuri, huna shida, na sisi serikali tunaahidi kuendelea kushirikiana na dini zote, kwa sababu serikali haina dini ila wananchi wake wana dini.

“Na niombe madhehebu ya dini nchini, wasemaji wenu wawe watu wa dini husika na si wanasiasa, kama ni Shehe azungumze Shehe kama ni Askofu azungumze Askofu, kama ni Padri au Mchungaji azungumze na huyo vinginevyo tunawapoteza waumini vibaya.

“Mkiwa na hao wasemaji ambao ni watu wa dini husika hata waumini watawasikiliza lakini kama wasemaji si watu wa dini husika, hata waumini hawatalipa jambo lenyewe uzito na wakati mwingine hao wasemaji ambao si wahusika wa dini wanaongeza chumvi na kuharibu jambo lenyewe,” alisisitiza Rais Magufuli.

Awali akikagua ujenzi wa jengo la Msikiti huo wa kisasa utakaokuwa pia na sehemu ya maduka ya bidhaa, kumbi za mikutano, chumba cha kuhifadhia maiti na Maktaba ya dini, Rais Magufuli alisema ujenzi huo umetokana na ombi lake kwa Mfalme wa Morocco aliyefanya ziara yake nchini mapema mwaka 2016.

Alisema katika ziara ya Mfalme huyo nchini, alimuomba kufadhili ujenzi wa msikiti mkubwa na uwanja wa michezo, jambo ambalo alikubali na kuahidi kujenga msikiti huo jijini hapo na kujengwa uwanja wa michezo mjini Dodoma.

“Mfalme wa Morocco alipokuja nchini nilimuomba mambo mawili, moja ni ujenzi wa msikiti mkubwa ambao watu watakwenda kumuabudu Mola wao na pili ni ujenzi wa uwanja wa michezo utakaojengwa Dodoma, nimekuja kukagua kimya kimya hata sikuwaambia Bakwata kama ninakuja, ila ujenzi unaendelea vizuri na niwapongeze kwa usimamizi mzuri,”alisema Rais Magufuli.

Baada ya kukagua ujenzi huo na kuridhika, Rais alichangia Sh milioni 10 kwa ajili ya kununua saruji mifuko 625, itakayosaidia ujenzi unaoendelea wa jengo jingine kwa ajili ya ofisi ya kisasa ya Bakwata.

Akizungumzia ujenzi huo, mkandarasi aliyekuwepo eneo hilo, Khalid Kijangwa alisema msikiti huo utakamilika ujenzi wake Aprili au Mei, mwakani.

Mara baada ya kumaliza ukaguzi huo, Rais aliwasalimu na kuzungumza na wananchi waliokuwa jirani na eneo hilo ambapo, mkazi mmoja alihoji kazi ya utambuzi wa mali za Bakwata umefikia wapi, ndipo Mufti Zubeir akasema baadhi ya mali zimeshaanza kurudishwa na kuwataka Waislamu kuwa wavumilivu na itapakofika wakati wa kuzungumza uamuzi wa mwisho waumini hao watataarifiwa.

Balozi wa Morocco nchini, Abdeliyah Benryane, alisema ujenzi huo umeanza kutekelezwa ,ikiwa ni ahadi ya Mfalme Muhammad VI na kwamba katika jengo hilo la msikiti kutakuwa pia na ofisi za Mfuko wa Mfalme huo utakaojulikana kama Muhammed Sis.

Katika hatua nyingine, Rais amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuhakikisha kipande cha barabara kinacholalamikiwa eneo la Kinondoni Shamba kwenda Biafra kinatengenezwa kwa fedha za Mfuko wa Barabara na ikikamilika barabara hiyo ipewe jina la Rashid.

Maelekezo hayo aliyatoa kutokana na Mjumbe wa Serikali ya Mtaa eneo la Kinondoni Shamba, kulalamikia ubovu wa eneo hilo na kumuomba Rais aangalie jinsi ya kuwasaidia wakazi wake.

“Mkuu wa Mkoa chukua namba ya simu ya huyu mzee, ni kiongozi mzuri anajali wananchi wake na barabara hiyo naagiza ijengwe kwa fedha za mfuko wa barabara na ikimalizika iitwe jina lake ‘Rashid Road’, alisema Rais Magufuli.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ameagiza ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi